Otile Brown akosoa pendekezo la Rais Ruto kwa Gen Z

“Tatizo tunapenda kupoteza mda na rasilimali nyingi kwa maneno, maneno matupu huleta hasara, maongezi ya nini tena?"

Muhtasari

•Otile alikosoa vikao vilivyopendekezwa kuwa ni ufujaji wa rasilimali na kutaka uwajibikaji kutoka kwa maafisa wa serikali.

•Rais alieleza nia yake ya kukutana na viongozi mbalimbali wa sekta zote wakiwemo vijana, viongozi wa dini na wengineo ili kujadili masuala ya kitaifa.

otile Brown
Image: instagram

Mwanamuziki Otile Brown ameelezea kutoridhishwa kwake na pendekezo la Rais William Ruto la kuunda baraza kutoka sekta mbalimbali kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na Gen Z, ambao wamekuwa mstari wa mbele katika maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha.

Kujibu maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha, yakiongozwa na Gen Zs, Ruto alitangaza kwamba hatatia saini mswada huo kuwa sheria.

Rais pia alieleza nia yake ya kukutana na viongozi mbalimbali wa sekta zote wakiwemo vijana, viongozi wa dini na wengineo ili kujadili masuala ya kitaifa.

Akiitikia wito wa Ruto wa vikao vya sekta mbalimbali, Otile Brown alisisitiza kuwa serikali tayari inajua nini cha kufanya ili kukabiliana masuala yaliyoibuliwa na vijana.

Alikosoa vikao vilivyopendekezwa kuwa ni ufujaji wa rasilimali na kutaka uwajibikaji kutoka kwa maafisa wa serikali.

“Tatizo tunapenda kupoteza mUda na rasilimali nyingi kwa maneno, maneno matupu huleta hasara, maongezi ya nini tena?? We all got job to do, kila mtu afanye kazi yake na wajibike.Sote tunajua cha kufanya,” Otile aliandika.

Mwimbaji huyo aliangazia haja ya kukabiliana na ufisadi, ambao aliutaja kuwa ni upotevu mkubwa wa fedha za umma, na kusababisha hasara nyingi.

“Tujifunze vizuri kusimamia nchi na mali, ufisadi umezorotesha maisha ya mwananchi ata wawekezaji wanatoroka, kazi zina pungua.

Ukitaka kumaliza deni la nchi yetu kwanza tuanze na hio karibia trilioni moja inayopotea kila siku.

Imagine kama hio pesa ingetengwa ingekua inalipa deni, hamgehitaji ata kuzidisha ushuru,” aliongeza.