Babu Owino aahidi kumsomesha mwanafunzi aliyeonekana akiuza mahindi usiku

Ametaka kusaidiwa kumtafuta msichana huyo ili aweze kumfadhili masomo yake na kuwasaidia wazazi wake kuanzisha biashara.

Muhtasari

•Msichana huyo alionekana akiuza mahindi akiwa amevalia sare ya shule  kando ya barabara katika eneo la Jomoko, barabara kuu ya Thika 

•Tukio hilo lilimfanya Babu Owino kukumbuka enzi zake akiuza pombe aina ya Chang'aa kwa maisha yake yote ya shule ya msingi na ya sekondari.

Babu Owino na msichana aliyekuwa anauza mahindi
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameahidi kufadhili masomo ya msichana anayekwenda shule ambaye alirekodiwa akiuza mahindi ya kuchemsha usiku.

Video ya msichana mdogo akiwa amevalia sare ya shule alipokuwa akiuza mahindi kando ya barabara katika eneo la Jomoko kando ya barabara kuu ya Thika ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mnamo Alhamisi, Julai 4, 2024.

Kupitia ukurasa wake Facebook,Babu Owino mnamo Ijumaa, Julai 5, 2024, aliomba usaidizi wa kumtafuta msichana huyo ili aweze kumfadhili masomo yake na kuwasaidia wazazi wake kuanzisha biashara.

Inasemekana kuwa msichana huyo huondoka katika Shule ya Msingi ya Kisiwa mjini Thika kila jioni kwenda kuuza mahindi hayo kando ya barabara.

Hata hivyo,Babu Owino alisimulia jinsi  tukio hilo lilimkumbusha wakati alipokuwa akiuza pombe aina ya chang’aa kila siku kutoka shuleni kwa maisha yake yote ya shule ya msingi na sekondari.