“Watu nyumbani kwetu Oyugis wanataka sana niwe MCA wao” – Stevo Simple Boy

“Watu nyumbani kwetu kule Oyugis wamekuwa wakitaka sana lakini nikasema wanipe muda kwanza nifanye muziki halafu nitakuwa MCA wao baadae. Mimi mwenyewe bado siko tayari,” alisema.

Muhtasari

• Kando na hilo la siasa, Stevo Simple Boy alisema ana msanii mpya ambaye anataka kumtambulisha na kumsaidia kutoboa kimuziki.

STEVO SIMPLE BOY
STEVO SIMPLE BOY

Msanii Stevo Simple Boy amedokeza nia yake ya kujitosa katika siasa kama njia moja ya kueneza huduma muhimu kwa mashabiki wake.

Simple Boy katika mahojiano, alifichua kwamba kwa muda mrefu amekuwa akipata shinikizo kutoka kwa watu nyumbani kwao Oyugis, kaunti ya Homabay wakimtaka kujitosa kwenye siasa ili kuwa kiongozi wao.

Rapa huyo wa ‘Mihadarati’ alisema kwamba japo hakuwahi kuwa na ndoto ya kuingia kwenye siasa, lakini huenda akajitosa ili kuitikia wito wa watu wake.

Hata hivyo, alisema kwamba kwa sasa amewaomba nafasi ya kufanya muziki na baadae atatathmini hilo la kuingia kwenye siasa kuwania wadhfa wa MCA.

“Watu nyumbani kwetu kule Oyugis wamekuwa wakitaka sana lakini nikasema wanipe muda kwanza nifanye muziki halafu nitakuwa MCA wao baadae. Mimi mwenyewe bado siko tayari,” alisema.

Kando na hilo la siasa, Stevo Simple Boy alisema ana msanii mpya ambaye anataka kumtambulisha na kumsaidia kutoboa kimuziki.

“Niko na msanii wangu pia ambaye natarajia kumsaini. Ni msanii wa injili na unajua kusema kweli miziki ya injili imedidimia sana hapa nchini, na huyu amekuwa akishikilia ujumbe wa injili tangu akiwa chipukizi mpaka hapa alipofikia,” Stevo alifichua sababu ya kumtafuta msanii huyo.