Magix Enga athibitisha kuhama Eldoret alikopelekwa na wahisani, ‘maisha ni kujisaidia mwenyewe’

Juzi, Enga alidokeza kwamba alipitia wakati mgumu wakati wa kushoot video ya wimbo wake ambapo ghafla alianza kutapika damu na kusema kwamba hawezi kumlaumu mtu yeyote bali yeye mwenyewe kwa matumizi mabaya ya pombe.

Muhtasari

• “Huyu ni mimi mwaka jana kupambana peke yangu na msongo wa mawazo mengi. Watu walinipiga picha nikiteseka" Enga alisema.

MAGIX ENGA
MAGIX ENGA
Image: FACEBOOK

Produsa Magix Enga amethibitisha kuwa hayuko mjini Eldoret tena, miezi kadhaa baada ya kuhamishiwa katika mji huo wa Bonde la Ufa na wahisani waliomnasua kutoka msongo wa mawazo uliosababishwa kwake na uraibu wa vilevi.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Enga ambaye juzi pia alithibitisha kuhangaishwa na uraibu wa pombe hadi kupelekea afya yake kukataa wakati anatayarisha video ya wimbo wake mpya, alisema kwamba kwa sasa hayuko tena Eldoret.

Mzalishaji huyo wa midundo aliyefahamika zaidi kwa midundo ya Gengetone hata hivyo alishukuru wahisani wema wakiongozwa na mtangazaji Mzazi Willy Tuva kwa kumsaidia na kumtafutia makazi mapya Eldoret ambapo pia alianza kufanya kazi na studio ya miziki ya Big Afric.

“Watu wanasema bado niko Eldoret kwa taarifa yako Siko huko nimefanikiwa kushoot video moja ya muziki wimbo wangu “Baba” ambao nilidhaminiwa na Mzazi Willy M. Tuva na studio ya Big Afric. Na nilifanikiwa kuwatengenezea nyimbo zaidi ya 10. Hongera wasanii wa Eldoret. Shukran sana msikate tamaa,” Magix Enga alifichua.

Produsa huyo ambaye pia ni msanii alichapisha picha yake ya mwaka jana wakati alikuwa katika hali mbaya ya unyongovu na kusema kwamba alijifunza kuwa katika maisha ni mtu mwenyewe tu anaweza kujisaidia, kwani aliona jinsi watu wengi walitumia hali hiyo yake kutafuta kiki nayo mitandaoni.

“Huyu ni mimi mwaka jana kupambana peke yangu na msongo wa mawazo mengi. Watu walinipiga picha nikiteseka lakini hiyo sio hoja yangu katika maisha haya unaweza kujiokoa tu mwenyewe. Niamini angalia wimbo wangu mpya wa Sishindani kwenye YouTube na niamini utapenda maudhui yangu,” Enga alisema.

Juzi, Enga alidokeza kwamba alipitia wakati mgumu wakati wa kushoot video ya wimbo wake ambapo ghafla alianza kutapika damu na kusema kwamba hawezi kumlaumu mtu yeyote bali yeye mwenyewe kwa matumizi mabaya ya pombe.