“Nilipoteza 10k followers Instagram kwa kuunga mkono Finance Bill” – Seneta Karen Nyamu

Nyamu alisema mmoja wa wafuasi wake alimtaka kujieleza kwa nini yeye kama mwanamke alikuwa anaunga mkono mswada wa fedha ambao ulikuwa na kipengele cha kuweka ushuru kwenye sodo.

Muhtasari

• “Kuzungumzia kuhusu habari potofu, mimi ni mmoja wa wale waliobeba mzigo wa habari potofu kuhusu mswada wa fedha, hata kwenye mitandao ya kijamii mheshimiwa Spika.”

KAREN NYAMU
KAREN NYAMU
Image: FACEBOOK

Seneta maalum Karen Nyamu kwa mara ya kwanza amevunja kimya kuhusu athari hasi ambazo zilimkumba haswa kwenye mitandao ya kijamii kufuatia msimamo wake wa kuunga mkono mswada wa fedha wa 2024.

Akizungumza katika kikao cha Seneti Jumanne, Nyamu alisema kwamba alipoteza zaidi ya wafuasi elfu 10 kwenye ukurasa wake wa Instagram baada ya kuonekana akipigia debe mswada huo tata ambao wengi wa Wakenya walikuwa wanaupinga.

Nyamu alisema kwamba mmoja wa wafuasi wake alimkabili kwenye upande wa kutoa maoni na kumtaka kujieleza kwa nini yeye kama mwanamke alikuwa anaunga mkono mswada wa fedha ambao ulikuwa na kipengele cha kuweka ushuru kwenye sodo.

“Kuzungumzia kuhusu habari potofu, mimi ni mmoja wa wale waliobeba mzigo wa habari potofu kuhusu mswada wa fedha, hata kwenye mitandao ya kijamii mheshimiwa Spika.”

“Nimepoteza zaidi ya wafuasi elfu 10 kwenye Instagram kwa sababu nilijiingiza katika mazungumzo kwenye Instagram ambapo msichana mmoja alikuja kwenye ukurasa wangu na kuniuliza kwa nini mimi kama mwanamke nilikuwa naunga mkono mswada wa fedha ambao ulikuwa unapendekeza kutoza ushuru sodo,” Nyamu alieleza.

Nyamu alijitetea kwamba alilazimika kujieleza kwa binti huyo na kumfafanulia kwamba hizo zilikuwa habari potofu kwani mswada wa fedha ulikuwa umependekeza ushuru kwa bidhaa za sodo ambazo zinatoka nje ya nchi pekee.

Nyamu alisema kwamba kutokana na maelezo yake kwa maswali kwenye Instagram yake, baadhi walimchukulia kama mtu mwenye kiburu na hata kumshtaki kwa rais wakati alikuwa na mazungumzo na vijana wa Gen Z kupitia jukwaa la X Space.

“Mheshimiwa Spika kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, nimeitwa mwenye kiburi kwa kuunga mkono msimamo wa serikali kwenye suala la mswada wa fedha. Wale wanaonijua, wale ambao tumejumuika nao watazungumzia kuhusu unyenyekevu wangu…” alijitetea.