Lavalava ajipata matatani msanii mwenza wa kike akimfungulia kesi mahakamani

“Huu ni wito wa mahakama kutoka kwa mlalamikaji kwenda kwa mlalamikiwa. Hiyo inahusiana na shauri ambalo mlalamikaji ambaye ni Lulu Diva, alifungua kesi mahakamani akiomba kulipwa zaidi ya milioni 200' wakili alisema.

Muhtasari

• Wakili wa Diva akizungumza na blogu moja, alithibitisha kwamba barua hiyo ni halali na mteja wake anataka fidia ya zaidi ya shilingi milioni 200 za Kitanzania kwa kuchafuliwa jina.

LALALALA NA LULU DIVA
LALALALA NA LULU DIVA

Msanii wa lebo ya WCB Wasafi, Abdul Juma Idd, maarufu kama Lavalava amejipata pabaya baada ya msanii mwenza, Lulu Diva kumfungulia kesi ya kumchafulia jina.

Katika barua hiyo ya mahakamani iliyotumwa kwake Lavalava, inadaiwa wiki mbili zilizopita alifanya mahojiano kwenye moja ya blogu na kutamka madai ambayo upande wa Diva uliyachukuliwa kuwa si ya kweli na ya kumchafulia jina lake.

Kipindi hicho, Diva kupitia kwa Instagram yake alichapisha ujumbe wenye aya ndefu akiteta jinsi matamshi ya Lavalava yalimlenga kwa njia hasi na kuahidi kuwa mkondo wa sheria lazima utafuatwa.

Kuna Muda Nakaa Kimya Ila Haimaanishi Mimi Ni Mjinga au Mpumbavu ila Naamua Kua kimya kwa Kulinda na kujiheshimu. Ila Sasa naona Naonekana kama Zoba kwa Kutaka kutrend kwenu kutumia Jina Au Maneno kuhusu Mimi nimechoshwa na nimechoka Tabia hizo ikiwemo Baadhi ya Media Na Wasanii Kwa kauli mbaya na za kuchafuliwa,” alisema.

“Nimesikitishwa Na Kauli za Msanii @iamlavalava Dhidi yangu zisizo na heshima Dhidi Yangu Nahisi Sasa Ni Muda Kila Mmoja Wa Kumheshim Mwenzie na Kutokuchukuliana poa , Sheria Itachukua Mkondo wake kwenye Hili...Na Mkome Mara Moja👆🏽Na Sio Ombi Ni Lazima,” Diva alichapisha.

Sasa imebainika kwamba Lulu Diva hakuwa anafanya mzaha na tayari barua ya mahakama imetumwa kwake Lavalava akitakiwa kuijibu ndani ya siku 21 la sivyo atafunguliwa mashtaka rasmi ya kumchafulia mtu jina.

Wakili wa Diva akizungumza na blogu moja, alithibitisha kwamba barua hiyo ni halali na mteja wake anataka fidia ya zaidi ya shilingi milioni 200 za Kitanzania kwa kuchafuliwa jina.

“Huu ni wito wa mahakama kutoka kwa mlalamikaji kwenda kwa mlalamikiwa. Hiyo inahusiana na shauri ambalo mlalamikaji ambaye ni Lulu Diva, alifungua kesi mahakamani akiomba kulipwa zaidi ya milioni 200 lakini pia na kuombwa msamaha kutokana na kauli ambazo mlalamikiwa kwa jina Lavalava alitoa wakati anafanya mahojiano Fulani na chombo cha mtandaoni,” wakili alisema.