Eric amtaka Ruto kuweka historia kwa kuteua mama mboga, watu wa boda kama mawaziri

“Kenyatta hakuwahi fanya hivyo, Moi, Kibaki na hata Uhuru wote hawakufanya hivyo. Ruto huenda akawa kama rais pekee Afrika ambaye atachagua mtu asiyejulikana na kumpa kazi ya uwaziri, kama kweli atafanya hivyo,” alisema.

ERIC OMONDI
ERIC OMONDI
Image: HISANI

Mwanaharakati Eric Omondi amempa changamoto rais William Ruto kuweka historia kwa mara ya kwanza katika taifa la Kenya kwa kuwateua watu wa uchumi wa chini katika baraza lake la mawaziri.

Akizungumza kwenye runinga ya Citizen asubuhi ya Ijumaa, takribani saa 12 baada ya rais Ruto kuvunjilia mbali baraza lake la mawaziri, Omondi alisema kwamba hii ni nafasi nyingine kwa rais kuweka historia ya kutimiza ahadi zake za kampeni.

Mwanaharakati huyo alimkumbusha rais Ruto kwamba wakati wa kampeni zake na uzinduzi wa manifesto yake miaka mitatu iliyopita, alijikita zaidi katika watu wa uchumi wa chini wakiwemo watu wa bodaboda, mama mboga, machinga na wachuuzi.

Alimkumbusha kwamba wakati ndio huu wa kuunda baraza lake jipya la mawaziri kwa kuwateua wachuuzi, machinga, bodaboda, mama mboga, watu wa mikokoteni na wale wa kufanya kazi duni kwenye mijengo.

“Nafikiri rais ameacha kuwasikiliza watu wake na ameanza kuwasikiliza watu, na kutoka upande wangu hiyo ni hatua nzuri. Ningependa kumpa changamoto rais kuweka historia sasa kwa vile ako na nafasi ya kufanyqa hivyo. Amevunja baraza lake na hatua inayofuata itategemea pakubwa. Ningependa kumuomba ateua watu wa bodaboda, mama mboga… kama njia moja ya kutimiza ahadi yake ya kampeni ya kutaka kuunda serikali ya mama mboga,” Omondi alisema.

Omondi alisema kwamba mama mboga na watu wa bodaboda wengi huku nje wana elimu ya kuwawezesha kuhudumu katika baraza la mawaziri.

“Kenyatta hakuwahi fanya hivyo, Moi, Kibaki na hata Uhuru wote hawakufanya hivyo. Ruto huenda akawa kama rais pekee Afrika ambaye atachagua mtu asiyejulikana na kumpa kazi ya uwaziri, kama kweli atafanya hivyo,” alisema.