“Mbona ni mimi tu kutoka Kenya nyimbo zangu zinavuma nje ya East Africa?” – Willy Paul

" Sijui ni kwa nini ni mimi tu msanii kutoka Kenya ambaye nyimbo zake zinavuma nje? Mungu bariki na wengine pia aaa! Lakini usipunguze Baraka za kwangu,” Willy Paul alisema.

Muhtasari

• Itakumbukwa msanii huyo alifanikisha moja ya kobalo kubwa zaidi kuwahi kutokea na msanii wa kimataifa, ‘I Do’ mwaka 2017 akimshirikisha msanii kutoka Jamaika, Alaine.

WILLY PAUL
WILLY PAUL
Image: INSTAGRAM

Msanii Willy Paul ambaye hivi majuzi alidokeza kuhamia Ujerumani amedai kwamba ni yeye tu msanii wa miziki ya kisasa kutoka Kenya ambaye nyimbo zake zinavuma na hata kupendwa zaidi nje ya mipaka ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Pozee, kama anavyojiita kimajazi, alichapisha ujumbe huo katika ukurasa wake wa Instagram akisema kwamba kila siku anawaombea wasanii wenzake kutoka Kenya kujisatiti na juhudi zao kuzaa matunda ili ngoma zao zipenye nje ya mipaka ya Kenya.

Pozee alionekana kutokuwa na jibu la kile alichodai kwamba ni yeye tu anavuma nje ya ukanda huu akitokea Kenya, swali ambalo aliuliza mashabiki wake.

Msanii huyo anayetamba na albamu ya Beyond Gifted, alisema kwamba amepata Baraka kupita kiasi na hata kufanya kufuru ya kumtaka Mungu kuelekeza Baraka hizo kwa wengine sasa, akisema kwamba yeye ni mfano bora na ulio hai ambao unafaa kufuatwa na wasanii wote wa Kenya.

“Wasanii wa Kenya wanastahili kutia bidii na juhudi kama Pozee, ndio msikike nje ya Afrika Mashariki kama Pozee. Sijui ni kwa nini ni mimi tu msanii kutoka Kenya ambaye nyimbo zake zinavuma nje? Mungu bariki na wengine pia aaa! Lakini usipunguze Baraka za kwangu,” Willy Paul alisema huku akidokeza mafanikio ya single yake mpya ya Lululala.

Pozee kwa mara nyingi amekuwa akijidai kuwa msanii wa Kenya ambaye amefanikisha mambo makubwa kimataifa, tetesi ambazo hata hivyo amekuwa akiambatanisha na ushahidi hai.

Itakumbukwa msanii huyo alifanikisha moja ya kobalo kubwa zaidi kuwahi kutokea na msanii wa kimataifa, ‘I Do’ mwaka 2017 akimshirikisha msanii kutoka Jamaika, Alaine.

Nyimbo hiyo ilimpakulia Pozee jina kubwa kimuziki na baadae akafanikisha kolabo na wasanii wengine akiwemo Harmonize, Rayvanny, miongoni mwa majina makubwa kwenye Sanaa ya miziki ya kisasa.