Muigizaji wa video za ucheshi Crazy Kennar kwa mara nyingine amethihirisha sababu ya kuwa moja ya vipaji vikubwa humu nchini.
Kennar, ambaye aghalabu hupata mawazo ya maigizo yake kutokana na matukio mbalimbali, safari hii amejikita katika suala zima la maandamano ya vijana wa Gen Z.
Kennar alifanya video yenye ujumbe pasi na kutumia maneno, akionyesha jinsi maafisa wa polisi hurejea katika maisha yao duni baada ya siku ndefu ya kukimbizana na waandamanaji hapa na pale.
Katika video hiyo, Kennar ambaye anaigiza kama afisa wa polisi wa kutuliza ghasia kwenye maandamano anafika katika makazi yake duni, kwenye nyumba ya mabati akiwa na mawanda yote ya kazi, ikiwemo sare, kifaa cha kujilinda dhidi ya ghadhabu ya waandamanji, vitoza machozi na vitu vingine ambavyo polisi hutumiwa wanapokuwa kwenye uwanja wa makabiliano na waandamanji.
Baada ya ‘afisa wa polisi’ kuingia katika nyumba yake ambayo haina umeme, anaanza kuwasha meko ya mafuta na kugundua haina mafuta na kisha kulazimika kutumia moto wa kuni.
Baada ya kumaliza kupika, anagundua hana maji ya kunawa mikono na hivyo kulazimika kutumia maji ya kuwasha ambayo walitumia kuwatawanya waandamanji barabarani, kisha anaketi na kuanza kula kabla ya kupokea simu kutoka kwa bosi wake akimhongera kwa kazi nzuri.
Kinaya ni kwamba bosi wake ambaye hakushiriki katika maandamano hayo anampa hongera huku yeye akisherehekea vinono na ‘afisa’ wake aliyehusika katika maandamano ya siku kutwa akila makapi kwenye nyumba duni.
Baada ya kula, ‘afisa wa polisi’ anajilaza kwenye kochi lake ambalo analitumia kama kitanda kisha kutumia kifaa cha kujilinda kama blanketi na kuanza kukabiliana na mbu ambao analazimika kutumia kitoza machozi kuwakabili ndani ya nyumba hiyo duni.
Video hii imewavutia wengi ambao wametafsiri ujumbe wa Kennar jinsi polisi wanaishi katika maisha duni kisha kutumiwa kuwatawanya wananchi ambao wanaandamana kupigania haki za kila mmoja, wakiwemo maafisa hao wa polisi.
Tazama video hiyo hapa;