Mchekeshaji kutoka Ukambani, Sammie Kioko amevutia maoni kinzani katika mtandao wa Instagram baada ya kutoa maoni yake kuhusu maandamano ambayo yamedumu kkwa mwezi sasa kushinikiza serikali kuwajibika katika masuala mbalimbali.
Kupitia insta story yake, Kioko alichapisha Jumatano akiomba Wakenya wanaoshiriki maandamano hayo, ambao asilimia kubwa ni vijana kama yeye kutathmini kusitisha maandamano sasa.
Kwa mujibu wa Kioko, anahisi maandamano hayo yamechagizwa sana na kugeuzwa kuwa vuguru, akidai pia kwamba yameanza kuchosha na kukera kwa wakati mmoja.
Kioko hata hivyo alifafanua kwamba si kufutiliwa mbali kabisa bali angependa vijana wachukue likizo kidogo ili kurejea baadae iwapo matakwa yao ambayo wamekuwa wakiibua katika wiki nne za maandamano yaliyopita hayatozingatiwa.
“Tunaweza angalau kusitisha maandamano haya? Nahisi kwamba yameanza kuchosha na kukera kwa wakati mmoja. Tupumzike kidogo, tutarejea baadae. Msinitumie salamu ni maoni tu,” Kioko alisema.
Maoni yake yalipokelewa kwa ukinzani mwingi, baadhi ya vijana wakitishia kumtumia salamu za matusi kwa kudai kwamba amelipwa na upande wa serikali kusema hivyo, huku wachache wakionekana kumuunga mkono.
Haya hapa ni baadhi ya maoni;
“Haaya ngoja sasa maombi tumekusamehe” Terence Creative.
“Sammie ukiendelea hivi tutakusalimia uso kama ovacado za ukambani” Meek Maleek.
“nani alikuambia uongee,,salamu zimeanza kufika au” vee1_ke
“Uko wapi apo me na mbogi yangu tukuje tukusalimie kidogo bro😂” breezlaboy.