Esther Chebet maarufu kama Star Chebet, aliyekuwa muigizaji katika kipindi cha runingani cha The Real Househelps of Kawangware ameibuka tena mitandaoni na kudai kwamba yuko tayari kuzipiga mnada akaunti zake zote katika mitandao ya kijamii.
Chebet, ambaye mwezi mmoja uliopita aliwashangaza watu kwa msururu wa jumbe za kutia wasiwasi kuhusu maisha yake kuchukua mkonod tofauti na kuingia katika kile alikitaja kama maisha ya kiroho amesema akaunti hizo zisipopata mteja kufikia mwisho wa mwezi anazifunga kabisa.
Chebet alisema kwamba anataka kupiga mnada akaunti yake ya Facebook yenye wafuasi 1.2m, akaunti ya Instagram yenye wafuasi 428k na ile ya TikTok yenye wafuasi 302k, akisisitiza kwamba ataziuza kwa yeyote atakayempa dau kubwa zaidi kuliko wengine.
“Watu wazuri wa Mtandao, ikiwa una nia, shiriki pendekezo lako na [email protected] wakubwa tu!’ alisema siku moja iliyopita.
Saa chache baadae, aliradidi akisema kwamba wengi wamejitokeza wakizitaka akaunti hizo lakini akasema hayuko tayari kuziachia kwa hela ndogo, akisema analenga ofa kubwa kabisa na ambayo iwapo itakosekana basi yuko radhi kuzifunga tu.
“Jambo, nilisema mnunuzi mwenye dau nono. Ni kama watu hamkunielewa, bila maswali mengi. Zikikosa wenyewe tunazifunga tu ifikapo mwisho wa mwezi,” aliradidi.
Mwezi mmoja uliopita, Chebet aliwatia mashabiki na marafiki wa karibu wasiwasi akidai kwamba alijikuta amefungua portal katika mto mmoja kaunti ya Kericho.
Kilichowatia wasiwasi mashabiki wake ni pale alipokiri kwamba katika utafutaji wa amani ya nafsi yake, alijipata amejiingiza kwenye baadhi ya mambo ya kiroho ambayo hawezi kujitoa… mambo ambayo hakuyatarajia.
“…maisha yamekuwa yakienda kasi sana... sijui mwisho wa siku nitakuwa sawa, lakini nilijiingiza kwenye kitu ambacho siwezi kukirudisha nyuma. Maisha ni ya kiroho; Nadhani nilijiingiza kwenye uhalisia usio sahihi katika utafutaji wangu wa amani ya akili na kuingia katika nguvu zisizo sahihi,” alisimulia.