Miezi kadhaa baada ya kuhama, mchekeshaji Mulamwah amewatembeza mashabiki wake kupitia kwa video akiwaonyesha mazingira ya mtaa mpya alikohamia.
Mchekeshaji huyo japo hakutaja jina la mtaa huo, lakini alisema kwamba ni sehemu nzuri na tulivu ikilinganishwa na mtaa duni wa Kariobangi alikokuwa anaishi ambako uhuni umekithiri.
Mulamwah alimshukuru Mungu kwa sehemu hiyo mpya, akisema kwamba alikotoka ni pabaya ambapo hata hangekuwa na nafasi ya kuchukua simu na kurekodi video kwa njia hiyo akiwa salama.
“Huu ndio mtaa na ile pale nyuma ndio nyumba ambako sisi tunaishi. Ni sehemu moja nzuri sana, namshukuru Mungu kwa eneo kama hili, mkiangalia mahali tumetoka na sasa hivi ni jambo la ajabu sana,” Mulamwah alisema huku akiwaonyesha mashabiki wake mandhari hayo.
“Huku pia barabara ni binafsi hivyo hutaona watu wakipita-pita, kuingia hapa unapita geti tatu. Manze ni God, nikilinganisha na Kariobangi, hata hii simu sasa hivi ingekuwa imeenda, lakini nashukuru tu Mungu kwa kunipa fursa ya kuweza kutoka kule baada ya muda kwa sababu inaonyesha watu kwamba inawezekana,” alisema.
Kuhusu jinsi alivyopata nyumba katika makazi hayo ya kifaharu, Mulamwah alisema;
"Ni eneo fulani tu zuri, siwezi sema ni wapi. Na hapa ni rafiki yangu fulani alinitafutia nyumba, unajua ukiwa ghetto ni vigumu kujua kama kuna nyumba za kuishi sehemu hizi."
Hata hivyo, Mulamwah alithibitisha kwamba hatoishi hapo kwa muda mrefu kwani pia ndoto yake ni kuhamia katika jumba lake la kifahari ambalo amekuwa akilijenga kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Mulamwah alifichua kwamba umaliziaji wa jumba hilo umekuwa ghali kuliko jinsi alivyokuwa akitarajia lakini akasema bado kazi inaendelea.
“Huku tu ni watu wako na boma zao binafsi, sisi tu ndio bado tunang’ang’ana pale lakini hivi karibuni tunatoka. Na nikizungumzia kuhusu kuhama, ujenzi wa nyumba unaendelea vizuri huko nyumbani lakini ni ghali kidogo kumalizia, sikuwa najua. Unakula ng’ombe mzima lakini kale kamkia ka mwisho ndio kila kitu,” alisema.