Mwimbaji wa nyimbo za Injili kutoka Tanzania Bonny Mwaitege hatimaye ameuzima uvumi kuwa ameaga.
Mwanamuziki huyo wa nyimbo mashuhuri kama vile: 'Mke Mwema' aliripotiwa kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani, tetesi ambazo zimezimwa na kukataliwa na mkewe.
Mkewe amethibitisha kuwa Mwaitege yuko hai na mwenye buheri wa afya.
Akizungumza naye Millard Ayo, mkewe Mwaitege alinukuliwa akisema "Bony Mwaitege ni mzima kabisa, ametoka safari ya Kenya na amefika nyumbani salama, amepumzika."
Mwimbaji wa nyimbo za KiKamba Stephen Kasolo naye amezima madai ya kifo cha Mwaitege bila kutarajiwa.
"Nimethibitisha kuwa Bonny Mwaitege yuko sawa, kuna mtu anatumiwa kuharibu jina lake na kusambaza habari za uongo. Wakenya tuache kupost habari zake, tumuombee na tuwaombee wanamuziki wengine pia."
Mwimbaji wa nyimbo za Injili kutoka Tanzania Christopher Mwahangila pia aliashiria uvumi huo kuwa habari za uwongo.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walikuwa wameripoti kuwa Mwaitege alikuwa akitoka kwenye tamasha la injili ajali hiyo ya uwongo ilipotokea.
Mwaitege anajulikana kwa nyimbo kama vile 'Sisi Sote' 'Mama Ni Mama' 'Maisha Ni Foleni' 'Utanitambuaje' miongoni mwa zingine.
Mwaitege alianza muziki kama mwimbaji wa nyuma na dansi katika bendi ya muziki ya Tanzania na baadaye akajitosa kama msanii wa kujitegemea.