“Unataka nifukuzwe kazi” Jalang’o akataa kusema bei ya saa yake ya mkononi

Jalang’o alionesha kutokuwa tayari kujikita katika kuzungumzia bei ya saa yake ya mkononi ikizingatiwa anga ya kisiasa ambayo kwa sasa inawakumbu wanasiasa wengi haswa kuhusu maisha yao ya fasheni na mali wanazomiliki.

Muhtasari

• Katika mahojiano siku chache kabla ya baraza la mawaziri kuvunjwa, Murkomen alikiri kwamba anamiliki saa ya laki 9, kiatu cha elfu 70 na mshipi wa karibia elfu 50.

MP JALANG'O
MP JALANG'O
Image: HISANI

Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor maarufu kama Jalang’o amekwepa swali alilokabiliwa na mwanahabari akilenga kujua bei ya saa yake ya mkononi.

Mbunge huyo wa ODM ambaye alitokea kwenye kipindi kinachoongozwa na mwanahabari Betty Kyalo kwenye runinga ya TV47 alidinda kutaja bei ya saa aliyokuwa nayo akisema kwamba atafutwa kazi.

Kyalo alianza kwa kumkaribisha kwenye kikao akisifia saa yake ya mkononi na kkwa utani kutaka kubaini bei yake lakini Jalang’o akacheka na kusema kwamba ni saa ya kawaida tu bila kutaja bei yake.

“[Akicheka] unataka nifukuzwe kazi, hii saa, si ya bei ghali sana, ni ya bei kiasi tu,” Mbunge huyo alisema huku akitania kwamba huenda pengine hata aliinunua miaka 10 au 30 iliyopita kabla ya kuwa mbunge.

Jalang’o alionesha kutokuwa tayari kujikita katika kuzungumzia bei ya saa yake ya mkononi ikizingatiwa anga ya kisiasa ambayo kwa sasa inawakumbu wanasiasa wengi haswa kuhusu maisha yao ya fasheni na mali wanazomiliki.

Wakenya wengi katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakionesha ghadhabu zao kutokana na maisha ghali ambayo viongozi wamekuwa wakionesha katika mitandao ya kijamii kwa kile wanahisi ni kuwaringia na pesa za mtoa ushuru.

Zogo hili baina ya wananchi wa maisha ya chini na viongozi wenye ladha nzuri katika fasheni imewafanya baadhi ya viongozi hao kuotesha vibarua vyao nyasi.

Wiki mbili zilizopita, aliyekuwa waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen alikuwa miongoni mwa waliopoteza kazi baada ya rais Ruto kulivunja baraza lote la mawaziri.

Wengi walionekana kufurahia mitandaoni kuhusu Murkomen kufukuzwa kazi kwa kile walidai kwamba alikuwa anaonyesha saa na suti ghali anazomiliki kaitka mtindo ambao haukuwafurahisha.

Katika mahojiano siku chache kabla ya baraza la mawaziri kuvunjwa, Murkomen alikiri kwamba anamiliki saa ya laki 9, kiatu cha elfu 70 na mshipi wa karibia elfu 50.