Msanii wa kizazi kipya Dufla Diligon ametoa wito kwa Wakenya kujitokeza kwa wingi na kufurika katika tamasha la injili la mwinjilisti Guardian Angel kama walivyoonyesha upendo kwa mwinjilisti kutoka Rwanda, Israel Mbonyi.
Diligon kupitia Instagram yake, alitoa wito kwa Wakenya kusambaza upendo walioonyesha kwa Mbonyi kama njia moja ya kumsapoti Mkenya mwenzao.
Msanii huyo kutoka Turkana alisema kwamba kwa muda mwingi ambao amekuwa kwenye tasnia ya Sanaa Kenya, amewajua Wakenya kama watu wenye hulka ya kukumbatia wasanii kutoka nje na kuwatelekeza wasanii wa humu nchini.
“Wale wote walioenda kwa tamasha la msanii kutoka Rwanda, Israel Mbonyi, tupatane pia kwa tamasha la Gospo 1 tusimame na Guardian Angel. Wakenya ni wazuri katika kutokea kwa matamasha ya wasanii wa nje lakini ikifika ni wakati wa msanii wao wanakwepa. Ninasubiri tujaze Sankara kwa ajili ya tamasha la Gospo1,” alisema.
Kwa ushirikiano wa mkewe Esther Musila, Guardian Angel amekuwa akipigia debe tamasha hilo lake kubwa ambalo litafanyika Jumamosi ya Agosti 17 katika mgahawa wa Sankara.