Brown Mauzo kufunga harusi na Kabinga mwaka 1 baada ya kutalikiana na Vera Sidika

Mauzo alisema kwamba mshawasha wa kumuoa Kabinga umepata msukumo zaidi kutokana na jinsi mrembo huyo amekuwa akimkosha kwa mapenzi yaliyo hai.

Muhtasari

• Sidika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka jana, alifichua kwamba yeye na Brown Mauzo si mtu na mpenziwe tena.

• Mauzo na Sidika waliweka wazi huba lao mwaka 2021 na katika kipindi cha miaka 3, walibarikiwa na watoto wawili.

Brown Mauzo na mpenzi mpya.
Brown Mauzo na mpenzi mpya.
Image: Instagram

Msanii wa kizazi kipya, Brown Mauzo amedokeza ujio wa harusi kubwa na mpenziwe wa sasa, Kabinga Jr.

Kupitia insta story, Mauzo alichapisha picha ya Kabinga akiwa amevaa rinda jekundu ba kusema kwamba vitu ambavyo amekuwa akimfanyia vimempa mshawasha wa kumuoa kabisa.

Mauzo alisema kwamba mshawasha wa kumuoa Kabinga umepata msukumo zaidi kutokana na jinsi mrembo huyo amekuwa akimkosha kwa mapenzi yaliyo hai.

 

Msanii huyo alimtaja Kabinga kama malaika akisema kwamba anazidi kutia dua kwa Mungu kutouzima huo moto wa kutaka kufunga ndoa naye.

 

"Huyu malaika ananipa mshawasha wa kutaka kuoa tena. Ninathibitisha. Hebu na tuwe na hafla kubwa hivi karibuni. Maombi yenu ndio tunahitaji," baba wa watoto wawili na Vera Sidika alifichua.

Kidokezo cha kutaka kufunga ndoa tena kinakuja ikiwa ni mwaka mmoja kamili tangu alipoachana na Vera Sidika.

Sidika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka jana, alifichua kwamba yeye na Brown Mauzo si mtu na mpenziwe tena.

Mwanasosholaiti huyo mama wa watoto wawili, Asia na Ice alisema kwamba iliwabidi kusitisha huba lao kutokana na kile alichokitaja kama ni kuchokana kimapenzi.

Mauzo na Sidika waliweka wazi huba lao mwaka 2021 na katika kipindi cha miaka 3, walibarikiwa na watoto wawili.