• Tamasha hilo pia litakuwa linaangazia kupongeza juhudi za maafisa wa polisi wa Kenya ambao walijiunga na wenzao nchini Haiti wiki kadhaa zilizopita.
• Kenya inalenga kutuma maafisa wa polisi wapatao 2,500 nchini Haiti na tayari makundi mawili ya polisi zaidi ya 500 wametua Haiti.
Rapa nguli wa Kenya Khaligraph atapata nafasi ya kipekee na adimu kutokea atakapojumuika na wasanii wengine kutoka mataifa ya kigeni katika tamasha la kuomba Amani na utulivu nchini Haiti.
Taarifa hizi zilifichuliwa na katibu katika wizara ya mambo ya nje, Korir Sing’oei kupitia ukurasa wake rasmi wa jukwaa la X.
PS Sing’oei alichapisha picha akimkaribisha Khaligraph Jones katika ofisi yake na kufichua kwamba atakuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha hilo la Amani chini ya alama ya reli #Harmony4Haiti.
Tamasha hilo pia litakuwa linaangazia kupongeza juhudi za maafisa wa polisi wa Kenya ambao walijiunga na wenzao nchini Haiti wiki kadhaa zilizopita kaitka juhudi za kuleta Amani katika taifa hilo la ukanda wa Carebbean.
“Sanaa na Utamaduni hutekeleza majukumu muhimu ya kuunganisha katika jamii yetu na ni nguzo muhimu za utangamano na uthabiti. Nilikutana na OG @KHALIGRAPH kutafakari tamasha lijalo la #Harmony4Haiti, linalolenga kuelewa na kuthamini kazi nzuri ya Jeshi la Polisi la Kenya katika Misheni ya Kimataifa ya Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa (MSS) nchini Haiti, ambayo hadi sasa imesajili matokeo ya kuvutia tangu kutumwa kwake,” PS Sing’oei alisema.
PS Sing’oei alifichua kuwa Khaligraph Jones atatumbuiza pamoja na wasanii wengine kutoka mataifa ya ukanda wa Carebbean na Romania, na humu nchini bila kutoa taarifa zaidi ukumbi ambao tamasha hilo litafanyika na tarehe kamili.
“Tamasha hilo litashirikisha wabunifu kutoka Kenya, Haiti, Romania, miongoni mwa nchi nyingine za Karibea, na litatoa mwanya wa kubadilishana kihistoria na kiutamaduni,” aliongeza Sing’oei.
Kenya inalenga kutuma maafisa wa polisi wapatao 2,500 nchini Haiti na tayari makundi mawili ya polisi zaidi ya 500 wametua Haiti na kuendeleza oparesheni ya kurejesha Amani katika mitaa ya mji mkuu, Port-au-Prince.