EXCLUSIVE

Chef Maliha Mohammed atangaza ujio wa shindano la kupika katika kaunti 5

Maliha alifichua kwa furaha kwamba shindano lake la kitaifa tayari limepata mfadhili (chapa ya kutengeneza unga) na timu ya wapishi watakaoibuka washindi kwenye fainali ya Oktoba 19 watakabidhiwa 100k pesa taslimu.

Muhtasari

• Maliha alifichua kuwa tayari wamefanya majaribio ya kupata timu ya kwanza itakayowakilisha kaunti ya Mombasa kwenye fainali.

• Majaribio hayo yalifanyika mnamo Agosti 10 na 11, ambapo washindi walikuwa ni mama na bintiye kwa majina Suhaila na Manthura.

• Majaribio yajayo yatafanyika katika kaunti ya Lamu mnamo Agosti 24 na 25 kutafuta wawakilishi wa kaunti hiyo ndogo ya Pwani katika fainali.

CHEF MALIHA
CHEF MALIHA
Image: HISANI

Mpishi maarufu kutoka ukanda wa Pwani ya Kenya, Maliha Mohammed ametangaza ujio wa shindano kubwa la kitaifa katika upishi.

Akitoa maelezo ya shindano hilo analoliita ‘National DUO Cooking competition’, Maliha alimwambia mwandishi wa Radio Jambo Moses Sagwe kwamba litafanyika katika kaunti 5.

“Ninaandaa shindano la kitaifa la kupika ambapo kaunti 5; Mombasa, Lamu, Kisumu, Nakuru na Nairobi, ambapo tunatarajia kupata timu ya wapishi wawili kila upande kumenyana kwenye fainali,” Maliha alisema.

Kuhusu jinsi ya kufanikisha usawa na uwazi katika shindano hilo, Mpishi huyo alisema;

“Hili ni shindano ambapo timu ya watu wawili itafanya kazi pamoja katika shindano la upishi. Nitatembelea kaunti hizo 5. Tunaanza na majaribio kisha mara tu washiriki watakapochaguliwa siku inayofuata ni shindano ambapo timu 1 pekee ndiyo itaibuka washindi wa kaunti hiyo ili kuiwakilisha kwenye fainali kuu mnamo Oktoba 19.”

Maliha alifichua kuwa tayari wamefanya majaribio ya kupata timu ya kwanza itakayowakilisha kaunti ya Mombasa kwenye fainali.

Majaribio hayo yalifanyika mnamo Agosti 10 na 11, ambapo washindi walikuwa ni mama na bintiye kwa majina Suhaila na Manthura.

Majaribio yajayo yatafanyika katika kaunti ya Lamu mnamo Agosti 24 na 25 kutafuta wawakilishi wa kaunti hiyo ndogo ya Pwani katika fainali.

Chef Maliha alifichua kwa furaha kwamba shindano lake la kitaifa tayari limepata mfadhili (chapa ya kutengeneza unga ya Pembe) na timu ya wapishi watakaoibuka washindi kwenye fainali ya Oktoba 19 watakabidhiwa 100k pesa taslimu na kupewa cheo ‘Kenya’s No.1 Duo Cooking Champs’.

Lakini je, ni nini kilimpa Chef Maliha motisha na msukumo wa kuanzisha shindano hili la kitaifa?

“Imepita miaka 10 tangu niingie kwenye shindano la uhalisia kaitka kupika. Niliibuka wa 3 nchini Kenya (Shindano la Royco fuata flava season 1) mnamo 2014. Sikupata kutambuliwa au chochote.  Ninahisi kuadhimisha miaka 10 ambayo niliamua kwa kuungwa mkono na marehemu mama yangu kabla ya kufariki dunia wiki moja kabla sijaingia kwenye shindano hilo.”

Maliha alisisitiza kwamba kando la wapishi kushindana katika kuonyesha ufundi wao jikoni, pia shindano hili linalenga kurudisha uhalisi wa utamaduni wa mapishi ya Kiafrika haswa vyakula vya Uswahili ambao umepotea katika kizazi cha sasa.

Umaarufu wa Chef Maliha ulipanda kimataifa mwaka uliopita baada ya kushiriki katika upishi akinuia kuweka rekodi mpya katika Guinness World Record, rekodi ambayo hata hivyo haikufaulu kusimama.

Alikuwa amepika kwa mfululizo wa saa 90 na majibu ya Guinness World Record yalidai kulikuwa na ukiukwaji wa masharti wakati wa mchakato wa upishi wake.