Musila afichua jinsi aliishia kuwa meneja wa muziki wa mumewe, ‘Haikuwa kuhusu mapenzi’

“Kwa hiyo, mimi kuja katika maisha ya Guardian haikuwa hata kuhusu uhusiano wa kimapenzi, lakini nafikiri Mungu na mipango yake mwenyewe alifikiria huyu ndio mke wake,” Musila alisema akitabasamu.

Muhtasari

• Alifichua kwamba kukutana kwao kwa mara ya kwanza hakukuwa kuhusu mapenzi bali alikuwa na tatizo na jinsi hakuwa anajulikana licha ya kuwa na miziki mizuri ya injili.

WAPENZI ESTHER MUSILA NA GUARDIAN ANGEL.
WAPENZI ESTHER MUSILA NA GUARDIAN ANGEL.
Image: FACEBOOK

Esther Musila amesimulia jinsi alijipata kuwa mmoja wa mameneja wakuu wa Sanaa ya mumewe, Guardian Angel.

Musila alizungumza na wanahabari baada ya kukamilika kwa tamasha la Gospo 1 lililoandaliwa na Guardian Angel usiku wa Jumamosi katika mgahawa wa Sankara, jijini Nairobi.

Alifichua kwamba kukutana kwao kwa mara ya kwanza hakukuwa kuhusu mapenzi bali alikuwa na tatizo na jinsi hakuwa anajulikana licha ya kuwa na miziki mizuri ya injili.

“Mume wangu ni mtu wa ajabu sana, wakati nilisikia wimbo wake kwa mara ya kwanza, swali langu la kwanza lilikuwa ‘ni nani meneja wake?’. Kwa sababu nilikuwa nafikiria huyu jamaa ako na talanta ya kipekee katika uimbaji, lakini mbona simjui? Kwangu mimi shida ilikuwa kwamba hakuwa anauzwa inavyofaa katika soko la Sanaa,” alisema.

“Kwa hiyo, mimi kuja katika maisha ya Guardian haikuwa hata kuhusu uhusiano wa kimapenzi, lakini nafikiri Mungu na mipango yake mwenyewe alifikiria huyu ndio mke wake,” Musila alisema akitabasamu.

Alimsifia mumewe kama mtu ambaye ana uchu na ari katika kile anachokitaka kukifanya na pia ni mtu ambaye hawezi kujiingiza katika jambo ambalo roho yake imemsuta.

“Langu ni kumshukuru Guardian Angel, ninajivunia sana uwepo wake na kwa msukumo wake kufanikisha tamasha la Gospo 1,” alisema.

Mwezi Juni mwaka jana, Guardian Angel alisema mkewe Esther Musila ni miongoni mwa timu ya watu 8 ambao wanasimamia kazi yake ya muziki.

Timu ya usimamizi pia inajumuisha meneja wa mitandao ya kijamii, mbuni wa picha, mpiga picha za video na mpiga picha.

"Ambacho watu wengi hawajui ni kwamba nina timu inayonisimamia ambayo inajumuisha mke wangu, watayarishaji wawili, wakili kati ya wengine. Lakini mke wangu ni meneja wangu? Kama si mke wangu, kazi yangu isingekuwa vizuri kama ilivyo hivi sasa.”

"Ni muhimu kuthamini mchango wake katika kazi yangu. Kuna tofauti kubwa ikiwa nitazingatia mahali nilipokuwa kabla ya kukutana naye na sasa. Namaanisha kwa mfano nilikuwa naishi Athi River, sasa hivi labda mimi ndiye msanii pekee wa injili ambaye anaishi Karen.”