• Kijana huyo kutoka kaunti ya Vihiga anayeishi mtaa wa Kangemi jijini Nairobi anadai ana urefu wa zaidi ya futi 8, jambo ambalo limefanya wengi kumpa jina la kimajazi kama ‘Gen Z Goliath’.
• Katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha habari, Marongo alisema hajawahi vaa kiatu kutokana na kukosa kupata kile kinachoweza kutoshea mguu wake mkubwa.
Director Trevor katika siku za hivi karibuni ameonekana akimpigia debe kijana anayejitambua kama mtu mrefu zaidi nchini Kenya, Bradley Marongo.
Trevor wikendi iliyopita kupitia Instagram yake aliendeleza wito wake kwa makampuni ya kibiashara nchini kutathmini kumpa Marongo dili kama balozi wao wa mauzo ili kutangaza biashara zao.
Mkurugenzi huyo wa blogu ya KOM alimtaja Marongo kama kivutio cha ajabu ambaye akitumiwa vizuri anaweza kuvuta faida kwa biashara nyingi ambazo zitajihusisha naye kama balozi wao wa masoko na mauzo kutokana na upekee katika kimo chake.
“Kwenu nyinyi makampuni ya kibiashara, tunayo mali ya kipekee na ya ajabu hapa nchini Kenya – Bradley, kijana wetu mrefu zaidi mwenye kimo cha futi 8. Kwa kufanya kazi naye, kampuni zenu si tu zitakuwa zinaonyesha shukrani halisi kwa talanta za humu nchini bali pia zitaonyesha utofauti wao katika soko lenye ushindani mkubwa la humu nchini,” Trevor alitoa rai.
Trevor alishauri kampuni hizo kufikiria kuchukua hakimiliki za picha zake ili kuzitumia kwenye mabango ya matangazo kutangaza biashara zao.
“Kwa kuanya hivi mtakuwa mmeonyesha kujituma kwa chapa zenu katika kuwatambua na kuwasherehekea Wakenya wenye upekee na kuwaweka katika nafasi ya mbele kama wanaosherehekea upekee wa Kenya,” aliongeza.
Marongo ambaye wengi walimtambua baada ya picha na video zake kusambaa mitandaoni wakati wa maandamano ya vijana dhidi ya serikali amekuwa gumzo pevu kutokana na kimo chake kirefu.
Kijana huyo kutoka kaunti ya Vihiga anayeishi mtaa wa Kangemi jijini Nairobi anadai ana urefu wa zaidi ya futi 8, jambo ambalo limefanya wengi kumpa jina la kimajazi kama ‘Gen Z Goliath’.
Katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha habari, Marongo alisema hajawahi vaa kiatu kutokana na kukosa kupata kile kinachoweza kutoshea mguu wake mkubwa.