• Nyota alihisi vibaya kuambiwa hivo na kuchapisha ujumbe wa hisia akimuombea mrembo huyo aliyedharau sura yake kuzaa mtoto anayemfanana
Msanii wa muda mrefu kutoka ukanda wa Pwani, Nyota Ndogo ameonyesha mafadhaiko yake kupitia ukurasa wa Facebook baada ya mtumizi mmoja wa mtandao huo wa kijamii kumtupia matusi ya kumsimanga.
Nyota Ndogo alichapisha video akionesha uso wake kabla ya mtumizi huyo wa Facebook kusimanga uso wake akisema kuwa ni sura iliyotangulia akhera.
Nyota alihisi vibaya kuambiwa hivo na kuchapisha ujumbe wa hisia akimuombea mrembo huyo aliyedharau sura yake kuzaa mtoto anayemfanana.
“Mshukuru MUNGU kakupa uzuri lakini kusema kuwa mimi uso wangu umetangulia akhera… hujafa hujaumbika ama umemaliza kuzaa? Basi hili ombi langu kutoka moyoni mwangu, ttakaposhika ujauzito upate mtoto afanane na mimi maana MUNGU hakosei,” Nyoto Ndogo alisema.
Pia alionyesha kukerwa na hulka ya watumizi wa mitandao ya kijamii mara kwa mara kuwa na mazoea ya kuwatukana watu maarufu.
Nyoto Ndogo alisema japo watu maarufu wengi wanaona matusi ya mahabiki na kutulia, lakini huwa wanaumia kwani hakuna mahali iliandikwa kwamba watu maarufu sharti watupiwe matusi.
“Kuna kitu nyinyi kama mashabiki zetu mnafaa mujue. Unaona hio damu inatembea kwenye mwili wako? Hio damu pia mimi inatembea kwenye mwili wangu.kuna mambo mengi mabaya yanaongewaga kunihusu mimi na najua hata wenzangu wanaojulikana wanayapitia.”
“Mimi na najua hata wenzangu wanaojulikana wanayapitia but mimi huwa napuuza. But haimaanishi hainiumi. Ndugu zangu mtu anaweza kukwambia kitu kikakuchoma ukalia ukarudi mtandaoni na tabasamu tu but msivuke mipaka mpaka mnatuumiza. Ama pengine mnafikiria hatuna majibu ama matusi?” Nyota Ndogo alihoji.