“Sijaacha kutafuta mapenzi na sitaacha kamwe!” Akothee atangaza uzinduzi wa kitabu kingine

Mada nyingine kwenye nembo ya nje ya kitabu hicho inatoa taarifa ya ukakamavu akisema kwamba hawezi kuchoka kuendelea na safari ya kutafuta mapenzi.

Muhtasari

• Msanii huyo alidokeza kwamba kitabu hicho kitasimulia maisha yake ya mihangaiko kutoka kutafuta mafanikio kimuziki, mapenzi na safari yake ya elimu.

AKOTHEE
AKOTHEE
Image: FACEBOOK

Mjasiriamali na msanii Esther Akoth maarufu kama Akothee amedokeza ujio wa kitabu chake kingine, miaka miwili baada ya kuchapisha kitabu chake cha kwanza.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee alichapisha muonekano wa nje wa kitabu hicho chenye mada ‘Turn your pain into purpose’ na kufichua kwamba sherehe ya kuzindia kitabu hicho itafanyika Oktoba 12.

Msanii huyo alidokeza kwamba kitabu hicho kitasimulia maisha yake ya mihangaiko kutoka kutafuta mafanikio kimuziki, mapenzi na safari yake ya elimu.

“Ni maumivu gani ambayo huwezi kuyaachilia na yanahisije kulia kuhusu mambo ambayo unafikiri huwezi kubadilisha, kwa nini unayabeba kila mahali? Je, tunaweza kutembea pamoja kupita maumivu yako kwa kusudi kuu?, Tukutane tarehe 12 Oktoba,” aliandika.

Mada nyingine kwenye nembo ya nje ya kitabu hicho inatoa taarifa ya ukakamavu akisema kwamba hawezi kuchoka kuendelea na safari ya kutafuta mapenzi.

Itakumbukwa msanii huyo licha ya kufunga harusi ya kufana Aprili mwaka jana, harusi hiyo haikudumu sana kwani miezi minne baadae ilisambaratika.

Akothee alifunga harusi na mwanamume raia wa Uswizi aliyempa jina ‘Omosh’ na licha ya kuweka maisha yao ya kimapenzi hadharani, wakati wa kuachana, walikaa kimya, mpaka pale Akothee alipopata ujasiri wa kuzungumzia kilichojiri wiki kadhaa baadae.