•Mwimbaji huyo ambaye anaaminika kwa sasa yuko Nigeria kutembelea familia ya mpenziwe alishiriki picha zake nzuri na mrembo huyo.
•"Natamani tungekutana mapema," Jux aliandika.
Staa wa Bongo, Juma Jux anaonekana kufurahia sana uhusiano wake mpya na mrembo kutoka Nigeria, Priscilla Ololufemi na hajakwepa kuuonyesha hilo waziwazi.
Jumatatu jioni, mwimbaji huyo ambaye anaaminika kwa sasa yuko Nigeria kutembelea familia ya mpenzi wake alishiriki picha zake nzuri na mrembo huyo.
Kwa upande wa maelezo, alifunguka kuhusu majuto ya kutokutana na Bi Priscilla mapema.
"Natamani tungekutana mapema," Jux aliandika.
Hili lilikuwa ni tukio moja tu ambapo staa huyo wa bongo fleva ameonyesha uhusiano wake mpya unaozidi kuimarika baada ya kuachana na mpenzi wake wa zamani.
Takriban miezi mitano iliyopita, Jux alithibitisha kwamba hayuko tena katika mahusiano ya kimapenzi na mrembo wake Karen Bujulu.
Katika mazungumzo na mtangazaji wa Wasafi, Lil Ommy, Juma Jux alithibitisha hilo na kusema kwamba yapata miezi mitatu sasa tangu kila mtu aanze kujishughulisha na hamsini za kwake.
“Ni kweli mimi na Karen [Bujulu] hatuko pamoja tena, imekuwa kwa muda sasa nadhani inaenda miezi 3 kama sio 4,” Juma Jux alithibitisha katika mahojiano hayo.
Kuhusu msanii mwenza Ommy Dimpoz kudaiwa kuwa chanzo, Jux alisema kwamba hata yeye alisikia madai hayo katika mitandao ya kijamii lakini hajapata kuthibitisha hilo.
Wiki chache zilizopita baada ya Jux na Bujulu kuonekana kufuta picha za kila mmoja kwenye kurasa zao Instagram na pia kutoonekana pamoja siku ya Wapendanao ya Februari 14, madai yaliibuliwa kwamba Ommy Dimpoz alimzunguka rafiki yake Jux kwa mpenziwe kupelekea kuachana kwao.
“Ommy Dimpoz ndiye alikuwa chanzo kama ambavyo ilisemekana, kuhusu Ommy, hicho ni kitu ambacho pia mimi nimekisikia kama ambavyo nyinyi mnavyosikia. Si kitu ambacho mimi najua au ninaweza sema sio au sicho,” Jux alisema.
Jux amekuwa si mwenye bahati katika mapenzi kwa miaka sasa tangu alipolipoteza penzi lake kwa mrembo Vanessa Mdee ambaye penzi lake liliota upya katika mtima wa msanii na muigizaji wa Marekani mwenye usuli wa Nigeria, Rotimi.