
Mwanahabari maarufu wa Kenya anayefanya kazi katika shirika la habari la
kimataifa la CNN, Larry Madowo, amemfichua mwanamke ambaye aliwasilisha ombi
lake la ndoa na hata kufuatilia ili kupata jibu.
Madowo mnamo Jumapili asubuhi alichapisha screenshot ya pendekezo la ndoa ambalo mwanamke huyo ambaye hakutambulishwa alimtumia mnamo Desemba 2023, na barua pepe nyingine alimtumia mnamo Oktoba 2024, akilenga kupata jibu kutoka kwake.
Katika barua pepe yake ya kwanza, mwanadada huyo alijitambulisha kama Mkenya mwenye umri wa miaka 24 ambaye angependa kuolewa naye.
“Siku njema Larry. Hakuna kupoteza maneno, mimi ni Mkenya wa miaka 24 na nataka unioe. Kila kitu kitaelezwa baadaye,” barua pepe ya kwanza ilisoma.
Katika barua pepe yake ya pili, mwanamke huyo alitaka kujua ikiwa mwandishi
huyo wa zamani wa NTV na BBC alikuwa tayari amepata jibu mwafaka kwake.
“Habari Larry. Marejeleo yanafanywa kwa barua pepe hapa chini. Hukunipa
jibu la ndiyo au hapana,” aliandika.
Barua pepe za mwanadada huyo ambaye hakutambulishwa zilionekana kumshangaza sana Larry Madowo na alikuwa na maneno machache tu juu yake.
"Hebu fikira ni nani aliyefuata pendekezo lao la ndoa?" Madowo alitoa maoni.
Hatua ya mwanamke huyo shupavu imezua maoni mengi juu ya chapisho la Larry
Madowo huku watu wakielezea maoni yao tofauti juu yake.
Ingawa
haijulikani wazi kama kwamba mwanahabari huyo mashuhuri yuko kwenye mahusiano,
amekuwa akihusishwa kimapenzi na mwanahabari mwenzake Edith Kimani.
Kwa muda mrefu, Wakenya wamekuwa wakidhani kwamba wawili hao wanachumbiana, kufuatia matendo yao ya wazi kwenye mitandao ya kijamii na matukio yao mazuri ya pamoja ambayo mara nyingi huwa wanashiriki hadharani.
Kuelekea mwishoni mwa mwezi Januari mwaka jana, Madowo aliamua kuwafanya mashabiki kukisia zaidi kwa ku-share post ambayo ilizidisha tetesi hizo kuwa yeye na Edith ni zaidi ya marafiki wa karibu.
Picha hiyo zuri iliambatana na nukuu fupi na tamu iliyosomeka, "Ikiwa sio hivi, sitaki📸 @gathigesest."
Na alichokuwa anakitaka Larry, ndicho alichokipata, kuzungumziwa. Chapisho hilo liliibua hisia mseto kutoka kwa mashabiki wake ambao waliamua kusherehekea 'uhusiano' kati ya nyota hao wawili wa habari.
Mapema mwaka uliotangulia, Edith alishiriki picha nzuri iliyoonyesha akimbusu Larry kwenye shavu lake na ujumbe mzuri kuhusu upendo wao kwa kila mmoja.
Edith alinukuu tukio hili,"Mwaka mpya. Same me. Bili sawa. Same love.@larrymadowo amechange wallet lakini, kwa hivyo matumizi mpya."
Wawili hao kwa muda mrefu wamekuwa wakidhaniwa kuwa wapenzi lakini hawakuwahi kuifanya rasmi.