
Kando na mambo mengi mazuri ambayo muziki umemletea ikiwa ni pamoja na pesa na umaarufu zaidi, mwimbaji Khalid Juma kwa jina maarufu Stoopid Boy amefunguka jinsi ambavyo muziki umekuwa na matokeo madhara katika maisha yake.
Akizungumza katika mahojiano ya hivi majuzi na Obinna TV, mwimbaji huyo wa kibao ‘G baga Jat’ alibainisha kuwa muziki umempelekea msongo wa mawazo.
Stoopid Boy alisema kuna shinikizo kubwa katika muziki na si rahisi kupambana nao, hasa bila elimu ifaayo.
“Muziki bila elimu inanipatia depression sana. Hii muziki inahitaji vitu mingi sana juu ata kuipanga bado inakupiga pressure,” Stoopid Boy alisema.
Mwimbaji huyo kijana pia alisimulia jinsi umaarufu kutoka kwa muziki wake umealika unyanyasaji na dhihaka kutoka kwa umma.
“Kama ukitembea hivi kwa barabara saa hizi mtaa kama Doni, mimi nimetoka hapo chini Ghetto, nikipita hivi naombwa pesa. Ukiambia mtu hauna hiyo pesa, ni matusi, wanasema ‘wee ni msanii mgani huna pesa?’. Nawaambiaje, wakati wangu utafika. Wacha kunipiga pressure na depression,” alisema.
Stoopid Boy alisema kuwa hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kufanya wimbo maarufu wa ‘G baga Jat’ ambao ulimpa umaarufu zaidi.
Alisema imekuwa ngumu kwake kuwa katika hali yake ya kawaida hadharani kwani anakumbana na kejeli nyingi kutoka kwa mashabiki.
“Tangu nitoe hiyo ngoma ata siwezi panda gari yangu ya 20 bob ya tao na Amani. Siku hizi nikiingia kwa mat wanauliza ‘huyu ni msanii mgani hana pesa?’” alisema.
“Lakini mimi nakuwanga nimejikubali juu nispojikubali nitajinyonga. Watu hawajui mimi hufikiria, vitu vingi sana. Mimi hujikubali ndo niavoid tu watu,” aliongeza.
Msanii huyo pia alizungumza kuhusu mpango wa kusitisha muziki kwa miezi kadhaa ili kuzingatia afya yake ya kiakili na kupambana na uraibu wa dawa za kulevya.
Aidha, alieleza jinsi ambavyo amekuwa akichukia muziki kwa masaibu ambayo umemletea.
“Muziki kwanza mimi nimeituliza. Muziki nimequit. Wasanii nyinyi ni wakali, nimewaachia muziki. Mimi kwanza sitaki mchezo na muziki, imenikasirisha, siipendi ata kidogo,” alisema.
Mwimbaji huyo pia alisema kuwa yuko tayari kufanyiwa ukarabati wa kitaalamu katika jitihada za kuacha madawa ya kulevya, na akaomba usaidizi kwa hilo..