Bahati aenda kimataifa, afichua anafanyia kazi wimbo na rapa wa Marekani Nicki Minaj

Bahati alitangaza kuwa wimbo huo ambao hakuutaja utatoka mwaka ujao.

Muhtasari

•"2023, Bahati na Nicki Minaj imethibitishwa..," alisema katika taarifa fupi ambayo alichapisha kwenye Instastori zake.

•Hapo awali Bahati aliwahi kudokeza mpango wa kufanya collabo na msanii mwingine maarufu wa Canada, Justin Beiber.

BAHATI
Image: HISANI

Mwimbaji  mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu Bahati amedokeza kuwa anafanyia kazi wimbo na rapa maarufu wa Marekani Nicki Minaj.

Katika taarifa yake ya Instagram, msanii huyo wa zamani wa injili alitangaza kuwa wimbo huo ambao hakuutaja utatoka mwaka ujao.

"2023, Bahati na Nicki Minaj imethibitishwa..," alisema katika taarifa fupi ambayo alichapisha kwenye Instastori zake.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa ujana ambaye anashabikiwa sana humu nchini hata hivyo hakufichua maelezo zaidi ya wimbo huo.

Nicki Minaj bila shaka ni mmoja wa marapa bora zaidi wa kike kote duniani na amekuwa kwenye sekta ya muziki wa kufoka kwa miaka mingi. Kwa upande wake, Bahati  alivuka hadi kwenye muziki wa kidunia takriban miaka miwili iliyopita baada ya kuwa katika tasnia ya muziki wa injili kwa miaka mingi.

Katika mahojiano na MC Jessy baada ya kuvuka kwenye muziki wa burudani, Bahati alisema kuwa kuacha muziki wa injili hakumaanishi imani na uhusiano wake na Mungu umefifia, alisema kwa kweli hata wameshikamana zaidi.

"Injili ni Kristo, nina Kristo moyoni mwangu na ninamwamini Mungu na yeye ndiye sababu ya mimi kuwa juu. Siwezi kumuacha Kristo lakini tasnia ya injili imeoza," alisema  mnamo mwezi Julai mwaka wa 2020.

Tangazo la Bahati la kufanya muziki na Nicki Minaj linajiri siku chache tu baada ya yeye kuachia kibao kikali cha mapenzi  'Abebo' ambacho alimshirikisha staa wa Ohangla Prince Indah. Hii ilikuwa mara ya pili ya wawili hao kufanya wimbo pamoja, takriban mwaka mmoja baada ya yao kufanya wimbo mwingine mzuri wa mapenzi 'Adhiambo' ambao umebaki akilini na moyoni mwa wengi tangu wakati huo.

Hapo awali Bahati aliwahi kudokeza mpango wa kufanya collabo na msanii mwingine maarufu wa Canada, Justin Beiber.

"Subirini hii, nitakuwa nafanya kitu na Justin Beiber, mtaona. Ngojeni tu," alisema.

Mume huyo wa Diana Marua alibainisha kuwa wimbo wake na Beiber   hautaharakishwa kwani staa huyo wa Pop anafanya kazi kwa ratiba ngumu.

Sawa, tusubiri wimbo wa Bahati na Nicki Minaj tunapoendelea kusubiri collabo yake na Justin Beiber ambayo alituahidi kitambo.