Baraka! Kambua atangaza ujauzito miezi 21 baada ya mwanawe kuaga

Mwimbaji huyo alipoiteza mtoto wake Malachi mnamo Februari 2021.

Muhtasari

• Kambua alitangaza habari za ujauzito kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alichapisha picha inayoonyesha tumbo lake lililochomoza.

Kambua
Image: Kambua Instagram

Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Kambua amefichua kuwa ni mja mzito kwa mara nyingine takriban miezi 21 baada ya kumpoteza mwanawe.

Kambua alitangaza habari za ujauzito kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alichapisha picha inayoonyesha tumbo lake lililochomoza.

Aliambatanisha na ujumbe wa kusherehekea huku akieleza furaha yake ya kubeba uja uzito baada ya kuwa na huzuni kwa muda mrefu.

"Anaturudishia amani. Anatuponya. Anafanya mambo yote kuwa mazuri 🦋," Kambua aliandika.

Miezi tisa iliyopita, mwimbaji huyo alimsherehekea mwanawe aliyeaga kwa kuandaa sherehe ndogo nyumbani kwake.

Alikuwa akiadhimisha mwaka mmoja tangu marehemu mwanawe Malachi Manundu kuaga dunia.

Kambua alifanya sherehe ndogo ndani ya nyumba na kuashiria hafla hiyo kwa maua na keki yenye maandishi 'For Malachi'.

"Heri ya siku ya kuadhimishwa mwaka mmoja mbinguni Malachi wangu wa thamani . Tungependa kukukumbatia leo, lakini najua Yesu na malaika wamekufunika kwa upendo mwingi na hiyo inatupa amani. Unapendwa milele " Kambua alimsherehekea mwanawe kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Kando na hayo amekuwa akiwahimiza watu kuwawajulia hali wanadada waliopoteza watoto wao na kuwasaidia kupambana na majonzi.

Katika chapisho lingine, alisema kuwa jeneza dogo ni zito zaidi ila hakutoa maelezo zaidi kuhusu kauli yake.

Kambua amewahi kujaliwa watoto wawili, wa kwanza anayejulikana kama Nate na Malachi ambaye alifariki siku chache baada ya kuzaliwa.

Siku ya akina mama mwaka huu, mwinjilisti huyo alisema kuwa ana hisia mbalimbali zilizokuja na siku hiyo.

“Kwa wanawake ambao hawajaweza kupata ujauzito wowote ila wamekuwa wakiona siku ya akina mama ikisherehekewa, wale ambao wamekuwa wakitamani zaidi ya mtoto mmoja kwa muda mrefu, wale wanaolea mtoto wa mwengine na kwa njia moja au nyingine mmeweza kuwadunisha kwa sababu ya hisia zinaowavunja, mnapendwa,” Kambua alisema.