Diamond Platnumz atoa sababu zake za kukataa kuteuliwa kuwania tuzo za Tanzania

Muhtasari

•Diamond alisema kwamba kiwango alichofikia sasa anapaswa kulinganishwa na wasanii kutoka mataifa mengine kwa kuwa hakuna yeyote aliyestahiki kushindana naye Bongo.

•Diamond alikosoa utaratibu unaotumiwa kuzawadi wasanii wa Bongo.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amesema hataki kulinganishwa na wasanii wengine wa Tanzania.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Diamond alidai kwamba kumlinganisha na wasanii wengine wa Tanzania ni kuwadhulumu.

Bosi huyo wa Wasafi alisema kwamba kiwango alichofikia sasa anapaswa kulinganishwa na wasanii kutoka mataifa mengine kwa kuwa hakuna yeyote aliyestahiki kushindana naye Bongo.

"Kuna vitu ukiniweka itakuwa haki nitamuonea mtu. Mimi sitaki kwa sababu mwisho wa siku utatengeneza ugomvi kati yangu naye. Kuliko mimi kugawanyika na Watanzania wenzangu, naona mara kumi heri nikashindane na mtu kutoka nje ili Watanzia wote tujumuike kwa pamoja tukapigane na wale ili ushindi ukije iwe faraja ya kila Mtanzania.. Mimi niko miongoni mwa wasanii watatu bora barani Afrika. Ukinishindanisha na mtu ambaye hata top 100 hayupo, unanikosea heshima yangu. Unakosea taifa heshima kwa sababu limetoa mwamba akashindane na wasanii wengine," Diamond alisema. 

Diamond pia alizungumzia suala la tuzo za kitaifa za wasanii wa Tanzania. Alisema kwamba anaziunga mkono tuzo hizo ila mwenyewe hataki kuteuliwa.

Mwanamuziki huyo alikosoa utaratibu unaotumiwa kuzawadi wasanii wa Bongo. Isitoshe, alidai kuwa haitakuwa haki kwa yeye kushindana na wasanii wenzake wa Tanzania kwa kuwa ana uwezo wa kunyakua tuzo zote.

"Ukiniweka nishindane na msanii wa Tanzania ni kama kumkandamiza msani mwenzangu kwa sababu hataniweza. Nina vigezo vingi vya kuhitimu. Niko na talanta, nina uwezo wa kifedha wa kujitangaza... Naona sio haki. Sitaki kuonekana mkubwa nyumbani. Sitaki kuonekana mkali Tanzania. Sitaki kuonekana mkubwa ama naweza kuliko msanii yeyote Tanzania. Nataka kuonekana naweza kuliko wasanii wa nje," Alisema Diamond.

Mbabe huyo wa muziki aliwasihi wasanii wenzake wa Bongo kuungana pamoja ili kukuza muziki wa taifa badala ya kuangazia ushindani.