Harmonize afunguka masaibu mengi aliyopitia katika safari ya kurudiana na Kajala

Staa huyo amefichua kuwa haikuwa rahisi kumshawishi Kajala kuhusu nia yake naye.

Muhtasari

•Harmonize amefichua kuwa wimbo wa sita katika albamu hiyo,  'Utanikumbuka' ulihamasishwa na mchumba wake Fridah Kajala Masanja.

•Amesema watu waliokuwa wamemzunguka Kajala wakati huo walikuwa wakimshauri dhidi yake wakidai alikuwa akitafuta kiki tu.

Harmonize na mchumba wake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize alizindua rasmi albamu yake mpya 'Made for Us' siku ya Ijumaa, Oktoba 28.

Albamu hiyo ya tatu ya Konde Boy ina jumla ya nyimbo kumi na nne na karibu kila wimbo una hadithi ya kipekee nyuma yake.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide amefichua kuwa wimbo wa sita katika albamu hiyo,  'Utanikumbuka' ulihamasishwa na mchumba wake Fridah Kajala Masanja ambaye pia ni meneja wake. Amesema mapambano aliyopitia kumshawishi muigizaji huyo amsamehe na akubali kurudiana naye ndiyo yalimfanya afanye wimbo huo.

"Nilitengeneza wimbo huo wakati wa kipindi cha 'nikubali tena'. Nilimbembeleza sana!! Nilifanya kila kitu kumuonyesha kiasi gani najutia na kiasi gani namhitaji tena," alisema kwenye Instastori zake siku ya Ijumaa.

Harmonize alifichua kuwa haikuwa rahisi kumshawishi mama huyo wa binti mmoja kuhusu nia yake naye kwa kuwa hata watu waliokuwa wamemzunguka wakati huo walikuwa wakimshauri dhidi yake wakidai alikuwa akitafuta kiki tu.

"Sasa tuko hapa na masiku yanayoyoma!! Mwaka unaelekea kukatika usichoke, usikatize tamaa, ndoto zako akikuelewa Mungu peke yake inatosha. Binadamu watakuelewa mbele ya safari!! " alisema.

Alisema aliifanya albamu hiyo akiwaza jinsi mchumba wake ambaye walikuwa wameachana naye wakati huo angemkumbuka.

Mapema mwaka huu, mwanamuziki huyo alitumia zaidi ya miezi miwili, mamilioni ya pesa na akalazimika kustahimili kejeli nyingi mitandaoni wakati akijaribu kumshawishi Kajala akubali kurudiana naye tena.

Hatimaye ombi lake la msamaha lilifaulu na wakarudiana mwezi Mei. Kwa sasa wawili hao wanatazamia kufunga pingu za maisha kwani Harmonize tayari amemvisha mchumba huyo wake pete ya uchumba.

Wachumba hao waliachana katika hali mbaya mwezi Mei mwaka jana na Harmonize akaripotiwa kuwa sababu ya utengano. Ilidaiwa walitengana baada ya Harmonize kujaribu kumtongoza bintiye Kajala, Paula.