Harmonize akiri upendo mkubwa kwa Christina Shusho na kubusu miguu yake

Harmonize alionekana akimkumbatia Shusho kabla ya kupiga goti na kubusu miguu yake.

Muhtasari

•Harmonize alilakiwa nchini na mtangazaji maarufu Maina Kageni ambaye alienda kumchukua Tanzania kwa ndege binafsi.

•Staa huyo wa Bongo alionekana akimkumbatia Shusho kabla ya kupiga goti na kubusu miguu yake.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Wikendi iliyopita, staa wa Bongo alikuwa nchini Kenya ambako alitumbuiza katika tamasha lililofanyika mjini Eldoret.

Harmonize alilakiwa nchini na mtangazaji maarufu Maina Kageni ambaye alienda kumchukua Tanzania kwa ndege binafsi.

Akiwa Kenya, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alipata fursa ya kukutana na mamia ya mashabiki wake Wakenya pamoja na watu wengine maarufu. Miongoni mwa watu maarufu  aliokutana nao ni mwimbaji mkongwe wa nyimbo za Injili Christina Shusho ambaye alikiri kuwa ni mwanamuziki wake kipenzi.

""Nimekutana na mwimbaji ninayempenda, OMG, Nampenda Christina Shusho. Nakufa kwa sauti yake," Harmonize alisema chini ya video ya mkutano huo wake na Shusho ambaye kwenye Instagram.

Katika video hiyo, staa huyo wa Bongo alionekana akimkumbatia Shusho kabla ya kupiga goti na kubusu miguu yake.

Shusho alionekana akijaribu kumwinua mwanamuziki huyo mwenzake wa Tanzania kabla ya wote wawili kufurahia mazungumzo mazuri.

Konde Boy alirejea nyumbani kwake Tanzania siku ya Jumatatu kufuatia tamasha la wikendi lililofanikiwa sana. Hata hivyo, anatarajiwa kurejea nchini Kenya wikendi ijayo kwa tamasha ambalo litafanyika Nairobi.

Kwa sasa staa huyo wa Bongo anaripotiwa kuwa single baada ya mpenzi wake Kajala Masanja kutangaza kutengana kwao.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema kupitia Instagram.

"Hakika nimekosea familia yangu, ndugu zangu, na marafiki zangu. Kutenda kosa si kosa, kosa kurudia kosa. Namsemehe X wangu na niko tayari kuenda kwa mwingine." 

Harmonize hata hivyo amesalia kimya kuhusu kutengana na Kajala Masanja licha ya shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wake  wakimtaka aweke wazi yaliyojiri kati yake na muigizaji huyo mkongwe wa Bongo.