• Harmonize amefunguka kuhusu hisia zake kuhusu msanii wake wa zamani Anjella kuzawadiwa gari na msanii wa WCB Zuchu.
•Harmonize aliwaomba Watanzania waendelee kuwaunga mkono wasanii wa kike wanaoinuana ili kuendeleza vitendo hivyo.
Bosi wa lebo ya muziki ya Konde Music Worlwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amefunguka kuhusu hisia zake kuhusu msanii wake wa zamani Anjella Tz kuzawadiwa gari na msanii wa WCB Zuchu.
Zuchu alimzawadia Anjella gari aina ya Subaru siku ya Alhamisi baada ya msanii huyo wa zamani wa Kondegang kufunguka kuhusu masaibu anayoyapata kwa kukosa gari.
Wakati akitumbuiza katika tamasha lililofanyika kisiwani Zanzibar Jumamosi jioni, Harmonize alipongeza kitendo cha Zuchu na kuweka wazi kuwa kilimfanya afurahi na kujivunia wasanii wa kike.
“Nataka kutumia nafasi hii kuwapongeza watu wa Zanzibar na mmemkuza msanii wa kike ambaye anafanya vizuri sana, Zuchu. Lakini jana katika pilkapilka zangu mitandaoni, niliona Zuchu kamzawadia gari Anjella. Kiukweli imenifurahisha sana kuona watoto wa kike wakishikana mkono wenyewe kwa wenyewe,” Harmonize alisema mbele ya mashabiki wake.
Staa huyo wa bongo fleva aliwaomba Watanzania waendelee kuwaunga mkono wasanii wa kike wanaoinuana ili kuendeleza vitendo hivyo.
Alhamisi usiku, Anjella alitoa shukrani zake baada ya mwimbaji mwenzake wa bongo Zuchu kwa kumzawadia gari jipya kabisa.
Zuchu alitimiza ahadi yake kubwa ya kumnunulia gari msanii huyo wa zamani wa Konde Music Worldwide, ambayo alimpa Jumatano.
Anjella ambaye alieleza wazi matatizo yanayomkabili kwa kutokuwa na gari hakuweza kuficha furaha yake wakati malkia huyo wa WCB akimzawadia gari jipya aina ya Subaru. Alizamia kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kueleza furaha yake na kumshukuru Zuchu kwa ishara nzuri aliyokuwa alionyesha.
“Napenda nafasi hii kukushukuru dada angu @officialzuchu ulichokifanya ni kikubwa sana tena sana umenipa nguvu ya kuinuka tena na umeipa faraja familia yangu wazazi nilikua napata shida sana kuhusu usafiri huu umeniipa gari nakushukuru sana dada angu,” Anjella aliandika kwenye Instagram.
Mwimbaji huyo mwenye sauti nzuri aliambatanisha taarifa yake na picha zake akipokea gari hilo jipya nyeupe Alhamisi jioni.
”Umenionesha upendo mkubwa sana, Mungu akuzidishie mafanikio zaidi na zaidi. Umenifanya nijihisi mpya katika hii dunia umenifanyia jambo kubwa sana katika kipindi ambacho sikua na tumaini lolote. Dada angu @officialzuchu nakupenda sana nakuombea mungu akupe maisha marefu na mafanikio zaidi❤️,” aliongeza.
Anjella ambaye awali alikuwa amesainiwa chini ya lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide kabla ya kuondoka mwaka 2022 alikuwa amefunguka masaibu ya kutokuwa na gari akiwa katika mahojiano na Diva The Bawse. Wakati akiwa kwenye lebo, alikuwa amezawadiwa gari na bosi wake, Harmonize.
Baada ya kutoka katika Kondegang, Anjella alilalamikia Harmonize kuchukua kila kitu alichokuwa amempa ikiwa ni pamoja na gari alilomzawadia.