Mwigizaji Tony wa Tahidi High afunguka kuhusu masaibu yaliyomkumba nusura ajitoe uhai

Muhtasari

•Baada ya kuondoka Tahidi High mwigizaji huyo alizamia kwenye kazi za serikali huku akifanya kazi katika wizara mbalimbali.

•Kutokana na masaibu chungu nzima ambayo yalikuwa yamemkumba, Tony alifanya maamuzi ya kuenda mbali na familia yake na kujitoa uhai.

Image: FACEBOOK// PRICNCE TSYDER

Mwigizaji wa zamani wa Tahidi High Patrick Gatundu almaarufu Tony amefunguka kuhusu maisha yake baada ya kupungia kipindi hicho kwaheri.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Tony alisema aliondoka Tahidi High baada ya miaka tisa kufuatia shinikizo la mashabiki.

Baada ya kuondoka pale mwigizaji huyo alizamia kwenye kazi za serikali huku akifanya kazi katika wizara mbalimbali.

"Vile tulitoka Tahidi niliingia gava. Nilikuwa dereva katika wizara ya Uchukuzi. Niliona ata nikiacha kuigiza siwezi kaa nyumbani lazima nifanye kazi. Kazi ya serikali ilinisaidia kiasi kwa sababu hiyo ndoyo niling'ang'ana nayo polepole. Changamoto ni kwamba nilikuwa maarufu alafu watu wananiona nikiendesha lori," Tony alisema.

Mwigizaji huyo alisema alifanya kazi kwa kipindi cha miaka kadhaa ila kadri siku zilivyosonga akaanza kupata hamu ya kurejea kwenye usanii.

Kutokana na hamu hiyo, Tony alijiuzulu na kuamua kutafuta kazi zingine. Hapo ndipo masaibu yalianza kumuandama kwani hata alishindwa kukidhi mahitaji ya familia yake ndogo. 

"Baada ya kujiuzulu kazi ya udereva, mambo yalianza kuwa magumu. Nilikuwa najaribu kutafuta kazi lakini sikuwa napata. Mke wangu ndiye alikuwa anagharamia mahitaji ya familia. Ilifika mahali akashindwa kustahimili. Ikawa ngumu, tulianza kukosana na kuvurugana," Tony alisimulia.

Kutokana na masaibu chungu nzima ambayo yalikuwa yamemkumba, Tony alifanya maamuzi ya kuenda mbali na familia yake na kujitoa uhai.

Mwigizaji huyo alifichua kuwa kilichokatiza mpango wake wa kujitoa uhai ni mtoto wa jirani ambaye alimtembelea wakati ambao  alikusudia kutekeleza mpango huo na kuutatiza.

"Nilisema nitatoka tu niende Mwea nijitia kitanzi stori iishe. Nilisema nitaenda mahali ata watu wakinitafuta hawatanipata. Sikuwa nataka kuachia watu shida niache wakiwa sawa. Nilipofika Mwea Mambo yalianza kubadilika. Siku ambayo nilikuwa nakusudia kujitoa uhai mtoto fulani alikuwa anashinda akinigongea mlango. Nilishindwa niaje. Ilifika mahali nikaona huyo ni Mungu alikuwa anaiongelesha. Nilifungua mlango akakaa hapo na hakuwa anaenda. Tulikaa hapo mpaka jioni. Niliamua sitajiua. Niliamua kuanza maisha upya," Alisimulia.

Baada ya hayo Tony alishauriwa na rafiki yake mzungu asafiri nje ya nchi katika juhudi za kutafuta utulivu wa akili.

Aliondoka na kuenda Ujerumani kwa kipindi cha miezi mitatu. Alisema kuwa akiwa Ujerumani alianza kuona maisha kwa mtazamo mpya na wazo la kujitoa uhai likamtoka.

Baadae alifunga ndoa na mzungu huyo aliyemshauri aende nje ya nchi.