Rayvanny azidiwa na upendo wa shabiki jukwaani hadi kumvisha pete

Rayvanny alimzawadi shabiki wake pete wakati wa tamasha ambalo alifanya Nakuru wikendi

Muhtasari

• Shabiki huyo alipanda jukwaani ambapo Rayvanny alikuwa akiwatumbuiza mashabiki na kumkumbatia mwanamuziki huyo.

• Rayvanny alifurahishwa na jambo hilo hadi kutoa pete aliyokuwa nayo na kumvalisha mwanadada huyo.

Rayvanny
Image: Rayvanny Instagram

Mwimbaji na mtunzi wa nyimbo za Bongo wa Tanzania, Rayvanny alimzawadi shabiki wake pete wakati wa tamasha ambalo alifanya jijini Nakuru wikendi.

Shabiki huyo alipanda jukwaani ambapo Rayvanny alikuwa akiwatumbuiza mashabiki na kumkumbatia mwanamuziki huyo.

Aliungana na staa huyo wa Bongo kuimba wimbo ambao alikuwa akicheza wakati huo huku akimuonyesha upendo.

Rayvanny alifurahishwa na jambo hilo hadi kutoa pete aliyokuwa nayo na kumvalisha mwanadada huyo.

"Umeipenda," alimuuliza shabiki huyo baada ya kumvisha pete hiyo.

Baada ya tukio hilo, Rayvanny na shabiki huyo walipigwa picha pamoja huku mashabiki wengine wakishangilia jambo la kusisimua alilofanya mwimbaji huyo.

Hivi majuzi  mwimbaji huyo, kupitia Instastori zake alidokeza kuwa anatamani kupendwa au kujitosa kwenye mahusiano. Chapisho hilo lilizua hisia mseto huku wanawake wengi wakimiminika kwenye DM zake na  kurusha mistari katika juhudi za kumtongoza.

"Jamani kama unajijua ni binti mzuri na unanifaa, tafadhali naomba, nitongoze," Rayvanny aliandika.

Rayvanny amewahi kuwa katika uhusiano hapo awali. Walakini, kinyume na wengi, alionekana kupendelea wanawake wamtongoze.

Hata hivyo haijafahamika kama ilikuwa kweli msanii huyo alikuwa na nia ya kujitosa kwenye mahaba au alikuwa anatafuta kiki kwa ajili ya wimbo wake mpya wa Nitongoze.

Katika wimbo huo, Rayvanny alishirikisha Staa wa Bongo, Diamond Platnumz.