Shoga Maxwell Mwamburi akiri kummezea mate msanii Jux

Alisema picha ya msanii huyo ambayo alipakia kwenye Instagram yake ilimletea bashasha mwilini mwake.

Muhtasari

• Maxwell alijitokeza hivi karibuni akisema yeye ni shoga na kubadili jina kujiita Maxine Hunty.

Maxine Hunty asema anamtamani kimapenzi Juma Jux
Maxine Hunty asema anamtamani kimapenzi Juma Jux
Image: instagram

Mwanaume shoga kabisa ambaye anatamba kwenye mitandao ya kijamii na mablogu, Maxwell Mwamburi ametema duku duku la moyo wake kwa kumtaja mwanaume ambaye amamtolea macho.

Mwamburi ambaye hivi juzi alijitokeza na kutangaza kwamba yeye ni shoga aliwataka watu kukoma kumuita Maxwell na badala yake akajibatiza jina la kike, Maxine Hunty.

Shoga huyo kutoka upande wa pwani alikuwa anazungumza katika mahojiano na mwanablogu na mchekeshaji 2Mbili ambapo alizungumza mengi pamoja na baadhi ya wanaume ambao anawamezea mate.

Maxine aliweka wazi kwamba hata kama wengi wamemjua kuwa shoga hivi karibuni ila amekuwa akicheza gemu lake chini ya maji kwa miaka kadhaa, sema alikuwa anaogopa kuweka wazi kutokana na hofu kwamba jamii itamtelekeza.

Vile vile, mwanamitindo huyo wa kiume alifichua kuwa amekuwa akichumbiana na mheshimiwa mmoja humu nchini kwa takriban miaka 7 sasa. Alisema mheshimiwa huyo ana mke na familia yake lakini yeye anaiheshimu nafasi yake kama mke wa pili, almaarufu nyumba ndogo.

Kulingana na yeye, tangia kitambo amekuwa akimmezea mate muigizaji wa filamu Nick Mutuma ila akasema kwa sasa ametoa hamu yake kwake kwani muigizaji huyo ametulia sana.

Alifichua kwamba kama kuna mtu ambaye kwa sasa anamnyima usingizi basi ni mwanafasheni na mwanamuziki kutoka Tanzania, Juma Jux.

“Juma Jux ananikalia vizuri sana. Kwanza kuna picha alipakia juzi akiwa kama nusu uchi vile, waah iliniwasha,” Maxine alisema.