“Tumieni akili!” Nyota Ndogo awakemea wanaokosoa sura yake na kuhoji alivyopata mzungu

Mwimbaji huyo aliwauliza wenye chuki walikotoa nguvu za kuchukia mtu wasiyejua.

Muhtasari

•Nyota Ndogo ameeleza kuchukizwa kwake na watu ambao  wamekuwa wakikosoa sura yake na kuhoji jinsi alivyoweza kupata mume mzungu mwenye pesa.

•Mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa hakuwahi kufuata pesa kwa mume wake mzungu, Bw Henning Neilsen.

Nyota Ndogo na mume wake Henning Neilsen
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki mkongwe wa Pwani Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amewasuta wanamitandao ambao wamekuwa wakimuonyesha chuki  licha ya kutomfahamu katika maisha halisi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nyota Ndogo ameeleza kuchukizwa kwake na watu ambao  wamekuwa wakikosoa sura yake na kuhoji jinsi alivyoweza kupata mume mzungu mwenye pesa.

"Siku moja mtu aliniuliza wewe Nyota ulivyo na sura mbaya na vile una pesa ingekua mimi ningefanya sajari, hapo ndio binadamu tumefikisha. Tumesahau mpaka aliyetuumba. Hii sura bado hamujaizoea tu? basi haiendi popote ulipo," alisema chini ya klipu ya video ambayo alipakia siku ya Jumatano.

Katika video hivyo, mama huyo wa watoto wawili aliwauliza watu wenye chuki walikotoa nguvu za kuchukia mtu wasiyejua.

Aliwashauri kutumia akili zao vizuri huku akiwabainishia kuwa sura sio kila kitu kinachohitajika kwa mafanikio maishani.

"Wengine mnaketi tu mkisema Nyota ana sura mbaya. Mnauliza aliwezaje kupata mzungu? Anakaa kienyeji!.. tumia akili ndugu yangu, akili hailetwi na sura. Wengine ata darasa la nane hatukukanyaga lakini Alhamdulillahi twashukuru Mwenyezi Mungu alitupatia akili. Tumesota tukiwa wadogo tukaogopa mpaka tukaanza kuwajengea future watoto wetu," alisema kwa hamaki kubwa.

Mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa hakuwahi kufuata pesa kwa mume wake mzungu, Bw Henning Neilsen.

Alisema hapo awali aliwahi kuwa kwenye ndoa na mtu asiyejaliwa pesa nyingi huku akieleza kuwa kila wakati anapojitosa kwenye ndoa huwa anafuata mapenzi wala sio pesa kama vile baadhi ya wakosoaji wake wamekuwa wakidai.

"Kule kwa wale maskini pia tulikuwa tunafuata mapenzi. Jameni wengine wetu tuna mapenzi ya kweli sio pesa. Ametokea wakati huu nimeangukia mapenzi kwa mtu mwenye pesa. Wewe wapenda mawe??" alisema.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya msanii huyo kumkaribisha nchini Bw Neilsen aliporejea kutoka nyumbani kwake Ulaya.

Jumanne, Nyota Ndogo alipakia picha akikulana denda na mzungu wake ndani ya gari la moshi la SGR.  Alisema kuwa hata hakuamini kufanya kitendo hicho cha faragha hadharani watu wakiwatumbulia macho mchana peupe.

“Nina furaha kukuona umerudi mfalme wangu, karibu nyumbani nilikuwa nimekukosa kinyama hata siamini tumebusiana kwa SGR watu wakituangalia, enyewe mapenzi ni kitu kizuri sana. Nakupenda mubaba wangu,”  alisema.