Wahu afunguka jinsi babake alivyomzuia kujitoa uhai baada ya kukumbwa na msongo wa mawazo

Msanii huyo alisema babake alimsaidia kupambana na masuala ya kisaikolojia alipokuwa kijana.

Muhtasari

•Wahu amefichua kuwa Bw Kagwi angeacha kazi yake ili tu kumtazama tu akishiriki katika hafla za shule.

"Kulikuwa na wakati kitu pekee ambacho kilinizuia kujitoa uhai ni jinsi baba yangu angenipeza, na kujilaumu mwenyewe " alisema.

Image: FACEBOOK// WAHU KAGWI

Mwanamuziki Wahu Kagwi ameandika barua ndefu ya shukrani kwa marehemu baba yake Bw Kagwi.

Katika barua hiyo iliyoandikwa kwenye ukurasa wake wa Facebook, mke huyo  wa Nameless amefunguka jinsi baba yake alivyokuwepo siku zote kwa ajili yake na ndugu zake walipokuwa wakikua.

Amefichua kuwa Bw Kagwi angeacha kazi yake ili tu kumtazama tu akishiriki katika hafla za shule kama vile michezo, tamasha za muziki na mijadala. Pia wangeshiriki muda pamoja kila wakati ambapo babake hakuwa kazini.

"Sasa vile mimi ni mtu mzima najiuliza alikuwa anamwambia nini bosi wake wakati tulipotoka kazini bila mpangilio kuja kunitazama nasoma shairi au kitu kingine," aliandika.

Mama huyo wa binti watatu alifichua kwamba yeye na baba walikuwa na uhusiano wa karibu sana na walikuwa wazi kwa kila mmoja kiasi cha kwamba walizungumza kuhusu karibu  kila kitu kilichokuwa kikiendelea maishani mwake.

"Tulizungumza kuhusu chochote na kila kitu; kuanzia kwa wavulana niliowapenda, shida zangu na kutojiamini, siasa, ndoto zangu, chochote tu. Tukawa karibu sana, hata nilipotaka kwenda club kwa mara ya kwanza, sikuweza kusema uongo, nilikuwa wazi naye. Ni wazi alikuwa na hofu juu ya hilo, lakini nilimwambia aamini jinsi alivyonilea. Aliniruhusu niende, lakini akamwambia kaka yangu mkubwa anisindikize," Wahu alisema.

Wahu alifichua kwamba babake pia alimsaidia kuhama na kukaa alipokuwa akianza maisha ya peke yake.

Pia alieleza jinsi mzazi huyo wake alimsaidia kupambana na masuala ya kisaikolojia alipokuwa kijana.

"Katika wakati wa giza tele maishani mwangu (nikiwa kijana) nilipopatwa na msongo wa mawazo(hadithi ya siku nyingine) kulikuwa na wakati kitu pekee ambacho kilinizuia kujitoa uhai ni jinsi baba yangu angenipeza, na kujilaumu mwenyewe 💔 💔"

Msanii huyo sasa ametoa wito kwa baba wote wa wasichana kuwasaidia binti zao  kihisia kama jinsi babake alivyofanya.

"Anahitaji kukubalika, kuhurumiwa, kupatiwa hakikisho, kutiwa moyo. Anahitaji muda wako," alisema Wahu.

Pia alitoa wito kama huo kwa baba wa wavulana na kueleza kuwa alisisitiza  zaidi kwa baba wa wasichana kwa kuwa yeye ni mzazi wa wasichana pekee.