Zuchu afichua mchango mkubwa wa mamake katika maisha yake, amtaka astaafu ili amtunze

Alidokeza kuwa mamake ndiye aliyekuza kipaji chake cha uandishi na uimbaji.

Muhtasari

•Katika ujumbe wake kwenye Instagram, Zuchu alimshukuru mama yake kwa mchango wake mkubwa katika maisha yake.

•Aliahidi kwamba ataendelea kutia bidii ili aweze kumpa gwiji huyo wa Taarab maisha mazuri anayostahili.

Khadija Kopa na binti yake Zuchu
Image: HISANI

Malkia wa Bongo Zuhura Othman Kopa almaarufu Zuchu amemsherehekea mama yake Bi Khadija Kopa.

Katika ujumbe wake kwenye Instagram, Zuchu alimshukuru mama yake kwa mchango wake mkubwa katika maisha yake.

Msanii huyo wa WCB alidokeza kuwa mzazi huyo wake ndiye aliyekuza kipaji chake cha uandishi muziki na uimbaji, na kumfanya aweze kuafikia ndoto yake ya kuwa mwanamuziki mkubwa ambaye yuko kwa sasa.

"Mpendwa mama, umenifundisha mema na kunikanya mabaya, ukanisindikiza kwenye safari ndefu ya ndoto zangu bila kuchoka. Bila yako nisingefika hata robio ya niliyonayo leo," Zuchu aliandika.

Msanii huyo kutoka Zanzibar alimshukuru mamake kwa kumuelewa na kuwa mvumilivu naye katika nyakati za aibu.

"Nakupenda sana malkia wangi Allah namuomba akuondoshee dhiki akupe furah ya milele. Bila ya wewe mimi ni nani," alisema.

Aliendelea kuahidi kwamba ataendelea kutia bidii ili aweze kumpa gwiji huyo wa Taarab maisha mazuri anayostahili.

"Natamani ustaafu ukae zako miguu juu ule kuku kwa mrija ila taratibu ndo mwendo. Allah yupo nasi kwenye hili. Kila dunia inavyozidi kuzunguka inanifunza kuwa wewe pekee ndo rafiki yangu na mimi nikwambie tu nakupenda rafiki wangu bora," alisema

Zuchu pia alimtakia malkia huyo wa Mipasho heri ya siku ya wanawake huku akimtaja kama mama mzuri zaidi duniani.

Huku akijibu, Bi Khadija Kopa alimshukuru kitinda mimba huyo wake na kumtakia neema ya Mungu juu ya maisha yake.

"Ahsante sana mwanangu kitindamimba. Mungu azidi kukupa Afya na Kheri zaidi," alisema.

Mwezi uliopita, Bi Kopa alifunguka kuhusu maisha yake tangu kufiwa na mume wake, ambaye ni baba yake Zuchu, takriban mwongo mmoja uliopita na kile anachokitazamia katika maisha ya siku za baadae.

Kopa alisema kuwa tangu mumewe kufa, hajawahi kupendana na mwanamume mwingine na akatangaza kuhusu mipango ya kutaka kurudi kwenye kidimbwi cha mapenzi na mwanamume aliyekomaa.

Alisema kuwa anatazamia kumpata mwanamume mkomavu, ikiwezekana aliye na miaka 50 kwenda mbele ambaye anajiweza vizuri pande zote kuanzia mfuko hadi masuala ya faraghani, na awe mcha Mungu.

Mimi jimbo liko wazi, tangu marehemu mume wangu afariki niko peke yangu. Mjumbe akija lazima awe na umri mkubwa, kuanzia miaka 50 kwenda juu, awe anajiweza anaweza kunitunza mimi mkewe sio yakhe sababu niko pale, akija tutasaidiana, shida zangu azijue, awe anamuogopa MUNGU awe mtu wa dini,”  alisema.

Kopa alisisitiza kuwa hana nia ya kulea kiben10 kwani nia yake ya kuzama mjini Dar es Salaam ni kutafuta pesa na kujitunza.