Mchekeshaji Awinja afunguka kuhusu harusi ya kitamaduni na mwenzake, Osoro Osoro

Wawili hao walidaiwa kufunga ndoa katika harusi ya kitamaduni iliyofanyika Jumamosi.

Muhtasari

•Mchekeshaji Awinja Nyamwalo ameweka wazi kwamba iliyodaiwa kuwa harusi yake ilikuwa ni mchezo wa kuigiza tu.

•Wawili hao walicheza densi pamoja na kundi la wanawake wazee walioigiza kama wapambe wa harusi yao.

walidaiwa kufanya harusi wikendi.
Osoro Osoro na Awinja Nyamwalo walidaiwa kufanya harusi wikendi.
Image: HISANI

Muigizaji Jacky Vike almaarufu Awinja Nyamwalo ameweka wazi kwamba iliyodaiwa kuwa harusi yake ilikuwa ni mchezo wa kuigiza tu.

Wikendi, muigizaji huyo wa zamani wa kipindi cha Papa Shirandula kwenye Citizen TV alidaiwa kufunga pingu za maisha na mchekeshaji mwenzake Osoro Osoro katika harusi ya kitamaduni iliyofanyika mahali pasipofichuliwa.

Siku ya Jumatatu hata hivyo, mama huyo wa mtoto mmoja alichapisha kipande cha kipindi cha 'Awinja's Perfect Wedding' (Ndoa  Kamilifu ya Awinja)  na kumwaga mtama kwamba harudsi ya wikendi haikuwa ya kweli.

"Je, wapambe wako wanaweza? Tuwapatie kadi yao ya bei? Imekuwa safari tangu kipindi cha kwanza cha #AwinjasPerfectWedding hadi kipindi cha mwisho, furahia!," muigizaji huyo alisema chini ya video aliyochapisha.

Katika video hiyo, Awinja na Osoro ambao wote walikuwa wamevalia vitenge vilivyolingana kwa rangi walicheza pamoja na kundi la wanawake wazee walioigiza kama wapambe wa harusi yao. Wanawake hao  ambao walikuwa wamevalia mavazi ya rangi ya zambarau na vijiti mikononi mwao walitikisa viuno vyao kwa mwendo wa taratibu huku watazamaji kadhaa wenye udadisi wakitazama.

Wachekeshaji hao ambao wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa muda mrefu walidaiwa kupeleka uhusiano wao katika hatua nyingine Jumamosi katika harusi ya kitamaduni ambayo ilipambwa na marafiki na wanafamilia  wa karibu.

Video zilizochukuliwa wakati wa hafla hiyo zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii, na kuibua hisia mseto kutoka kwa mashabiki na wafuasi wao.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walipuuza madai ya harusi hiyo, wengi wakisema kwamba huo ni mchezo mwingine wa vichekesho.

Kutokuwepo kwa marafiki mashuhuri wa wawili hao kwenye hafla hiyo ya kitamaduni kulieleza mengi kuhusu uhalisi wake. Hii ilifanya iwe vigumu kwa mashabiki kuamini kwamba kweli Osoro na Awinja walikuwa wamefunga ndoa.

Kwa muda mrefu zaidi sasa, wachekeshaji hao wawili wamekuwa wakicheza mume na mke katika michezo yao mingi ya kuigiza - na hilo lilifanya iwe vigumu kwa mashabiki kuamini kuwa wao ni wapenzi.