"Mimi ni bingwa wenu" Ezekiel Mutua aahidi kuwapigania na kuwatajirisha wanamuziki wa Kenya

Muhtasari

•Mutua alitangazwa kama mkurugenzi mtendaji mpya wa MCSK siku ya Jumanne, takriban miezi saba baada yake kutimuliwa KFCB.

•Mutua amesema yupo tayari kupigania wanamuziki, kulinda haki zao na kuyapatia madai yao kipaumbele.

Bosi mpya wa MCSK Ezekiel Mutua
Bosi mpya wa MCSK Ezekiel Mutua
Image: FACEBOOK// EZEKIEL MUTUA

Mkurugenzi Mtendaji  mpya wa Jumuiya ya Hakimiliki ya Muziki ya Kenya (MCSK), Bw. Ezekiel Mutua ametoa hakikisho kwa wanamuziki kwamba atashirikiana nao vizuri ili kuupeleka mbele muziki wa Kenya.

Katika taarifa yake ya Jumanne, Mutua amesema yupo tayari kupigania wanamuziki, kulinda haki zao na kuyapatia madai yao kipaumbele.

Bosi huyo wa zamani wa Bodi ya Uainishaji wa Filamu nchini Kenya MCSK)  pia ameahidi kuheshimisha wanamuziki wa Kenya na kufanikisha utajiri wao.

"Kwa wanamuziki wote wa Kenya, ujumbe wangu ni rahisi: Nitawafanyia kazi nanyi na niwafanyie kazi ili kufanya muziki uwe wa faida na wa maana. Nitawapigania, nitatetea haki zenu na kupatia mazungumzo kuhusu muziki kipaumbele kama nilivyofanya na filamu. Kwa pamoja tutainua ubora wa muziki wa Kenya na kurejesha utukufu uliopotea wa tasnia hii. Mimi ni bingwa wenu. Katika nchi zinazoendelea zaidi, wanamuziki ni miongoni mwa watu matajiri zaidi na wanaoheshimika zaidi katika jamii. Inaweza na itatokea nchini Kenya pia!" Mutua alisema.

Bosi huyo amewasihi wanamuziki kumuunga mkono ili kufanikisha kazi yake katika idara ya MCSK.

"Kwa Bodi ya Wakurugenzi ya MCSK, wafanyakazi wenzangu wazuri ambao nimekutana nao kufikia sasa, kwa wadau wetu wote, kwa marafiki na mashabiki wangu, asante kwa mapokezi mazuri!" Taarifa yake ilisoma.

Mutua alitangazwa kama mkurugenzi mtendaji mpya wa MCSK siku ya Jumanne, takriban miezi saba baada yake kutimuliwa KFCB.