Mjasiriamali Pancras Karema asherehekea mafanikio yake makubwa akiadhimisha siku ya kuzaliwa

Alitoa shukrani zake kwa kila mtu ambaye amekuwa sehemu ya safari yake wakiwemo marafiki, familia na wateja wake.

Muhtasari

•Mjasiriamali huyo alitoa shukrani zake kwa kila mtu ambaye amekuwa sehemu ya safari yake wakiwemo marafiki, familia na wateja wake.

•Hivi majuzi, Karema alifichua kuwa wazo la kuanzisha kampuni ya utalii lilitokea wakati yeye na mwanzilishi mwenzake walipokuwa wanaendelea na masomo katika chuo kikuu..

Mjasiriamali Pancras Karema

Mjasiriamali mashuhuri wa Kenya, Pancras Karema amesherehekea mafanikio yake makubwa katika ulimwengu wa biashara anapoadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Karema ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Expeditions Maasai Safaris anaadhimisha siku yake maalum hivi leo, Novemba 20 na amemshukuru Mungu kwa mafanikio yake.

Wakati akisherehekea kupiga hatua moja mbele, mjasiriamali huyo alitoa shukrani zake kwa kila mtu ambaye amekuwa sehemu ya safari yake wakiwemo marafiki, familia na wateja wake.

“Leo ninaposherehekea siku yangu ya kuzaliwa, nimefurahi sana. Asante Mungu kwa kuniongoza katika safari hii ya ajabu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Expeditions Maasai Safaris,” Karema alisema.

Aliongeza, "Familia yangu imekuwa mwamba wangu, sapoti yao isiyoyumba huchochea safari yangu kila siku. Kwa wenzangu katika Expeditions na marafiki, kunitia moyo na kuniamini kunamaanisha yote kwangu.”

Bw Karema alikuwa na maneno mazuri kwa wateja wao akikiri kuwa safari yake isingefanikiwa bila uungwaji mkono wao.

“Kwa wateja wetu wazuri, imani na matukio yenu ya kusisimua 🌟🦒 imefanya safari hii kuwa ya ajabu sana. Asanteni kwa kutufanya nambari moja na kwa kuwa sehemu ya hadithi hii nzuri! Asanteni sana kutoka chini kabisa ya moyo wangu 🙏,” alisema.

Makumi ya wanamitandao wakiwemo watu mashuhuri pia walijitokeza kumsherehekea mjasiriamali huyo ambaye kila uchao, amekuwa akipiga hatua kubwa katika ulimwengu wa biashara.

Mchekeshaji Desagu alisema, “Nisaidieni kumtakia siku njema ya kuzaliwa Bw Pancras Karema pale best tour and travel company @expeditionsmaasaisafarisltd. Unaweza kupata ziara ya bure kwa marudio ya ndoto yako."

Bw Pancras Karema alianzisha Expeditions Maasai Safaris pamoja na Lawrence Gitonga takriban miaka minane iliyopita na kampuni hiyo ya utalii imeendelea kukua siku baada ya siku.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Bw Karema alifichua kwamba wazo la kuanzisha kampuni ya utalii lilitokea wakati yeye na mwanzilishi mwenza wake walipokuwa wanaendelea na masomo chuoni.

"Sote wawili tulipenda urembo wa Kenya tangu enzi za utoto wetu, tulikua karibu na msitu wa Mlima Kenya ambapo tulikuwa tukienda kisiri ili kujivinjari," Bw Karema aliambia Business Daily.

Karema ambaye ana Shahada ya Kwanza katika Usimamizi wa Utalii na Ukarimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi alifichua kuwa walianza kampuni hiyo wakiwa na mtaji wa awali wa takriban Ksh. 10,000 ambapo yeye na mwenzi wake walichangia Ksh5000 kila mmoja.

Kampuni hiyo sasa ina wafanyakazi zaidi ya 50 na inapata wateja kutoka duniani kote.