Mr Seed apambana na majeraha kuhudhuria mazishi ya rafikiye, aangua kilio kaburini mwake (+picha)

Mwimbaji huyo alionekana akilia kwenye eneo la kaburi la marehemu baada ya kuzikwa shambani mwao.

Muhtasari

•Mwimbaji huyo ambaye alionekana kuwa na maumivu makali alijitahidi kabisa na kuhudhuria mazishi hayo ya Jumamosi.

•Mr Seed ametangaza kuwa atachukua mapumziko kutoka kwenye mitandao ya kijamii ili kuangazia afya yake ya mwili na ya kiakili.

awezwa na hisia wakati wa mazishi ya mpiga picha wake Ambrose Khan katika eneo la Igembe North mnamo Jumamosi, Mei 6, 2023.
Mr Seed awezwa na hisia wakati wa mazishi ya mpiga picha wake Ambrose Khan katika eneo la Igembe North mnamo Jumamosi, Mei 6, 2023.
Image: HISANI

Mpiga picha za video, marehemu Ambrose Mburu Andrew almaarufu Ambrose Khan hatimaye alizikwa siku ya  Jumamosi nyumbani kwao katika eneo la Igembe Kaskazini, kaunti ya Meru.

Makumi ya waombolezaji wakiwemo wanafamilia, marafiki na washirika wengine wa karibu walihudhuria mazishi kutoa heshima za mwisho.

Mwelekezaji huyo maarufu wa video alifariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea katika barabara kuu ya Nairobi-- Naivasha ambayo pia iliwahusisha wasanii wengine kadhaa ambao walikuwa pamoja naye.

Mwimbaji wa nyimbo za injili na za mapenzi, Moses Tarus Omondi almaarufu Mr Seed ambaye alikuwa akisafiri pamoja na marehemu Ambose mnamo siku ya ajali aliugua majeraha mabaya na amekuwa akihudumiwa na wahudumu wa afya. Licha ya kujeruhiwa, msanii huyo wa zamani wa EMB ambaye alionekana kuwa na maumivu makali alijitahidi kabisa na kuhudhuria mazishi hayo ya Jumamosi.

Wakati wa maziko hayo, Mr Seed alionekana akihangaika kusimama na kutembea  alipoombwa kuwasalimia waombolezaji. Pia alionekana akilia kwenye eneo la kaburi la marehemu baada ya kuzikwa shambani mwao.

Baadaye, kwenye ukurasa wake wa Instagram, alipakia picha yake akiwa amesimama kando ya jeneza la Ambrose na kueleza jinsi alivyoumizwa na kufariki kwa mshirika wake wa karibu.

Wakati huohuo, aliwafahamisha mashabiki wake kuwa atachukua mapumziko kutoka kwenye mitandao ya kijamii kwa muda ambao haujawekwa wazi ili kuangazia afya yake ya mwili na ya kiakili.

"Ninatoka kwenye mitandao ya kijamii kwa muda, nahitaji kujishughulisha na afya yangu/akili yangu. Nitarudi hivi karibuni. Baraka. Nawapenda mashabiki wangu, tuonane hivi karibuni," aliandika kwenye Instastori zake.

Marehemu Ambrose alikuwa kwenye gari moja na Mr Seed, DK Kwenye Beat, mpiga picha mwingine na mfanyabiashara wakati wa ajali.Yeye ndiye mtu pekee aliyekuwa kwa  gari hilo ambaye alipoteza maisha huku wengine wawili waliokuwa kwa gari ambalo waligonga nalo wakifariki dunia pia.

Wakati akitangaza kifo chake, mkewe Mr Seed, Nimo Gachuiri alieleza kuwa walisikitishwa na kifo cha Ambroze kwa kuwa alikuwa rafiki wa karibu. Wawili hao walionekana kuumia moyo sana wakati wa mazishi.