Mwanahabari Willis Raburu azungumza baada ya kupoteza kilo 40 kufuatia upasuaji

Kwa mujibu wake, Raburu amepoteza uzito mkubwa wa mwili kutoka kilo 164 hadi kilo 124.

Muhtasari

•Raburu alifanyiwa upasuaji wa gharama kubwa wa  gastric bypass mwezi Agosti mwaka jana kwa lengo la kupunguza uzito.

•Raburu alionyesha mwonekano wake mpya takriban miezi tisa baada ya kufanyiwa utaratibu huo na kuonyesha jinsi anavyojivunia maendeleo hayo makubwa.

Image: INSTAGRAM// WILLIS RABURU

Mwanahabari na mtumbuizaji maarufu Willis Raburu amefichua kwamba amepoteza kilo 40 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Willis Raburu alifanyiwa upasuaji wa gharama kubwa wa  gastric bypass mwezi Agosti mwaka jana kwa lengo la kupunguza uzito wa mwili wake na ni dhahiri kuwa utaratibu huo umezalisha mafanikio makubwa.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, mtumbuizaji huyo alionyesha mwonekano wake mpya takriban miezi tisa baada ya kufanyiwa utaratibu huo na kuonyesha jinsi anavyojivunia maendeleo hayo makubwa.

"Maendeleo. Fanya kile kinachokufurahisha. Wekeza ndani yako zaidi na zaidi. Unastahili," alisema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Aliongeza, "Unateseka peke yako na kwa hivyo ni wewe pekee unayejua. Sherehekea na ujitunze. Una wewe tu."

Kwa mujibu wake, Raburu amepoteza uzito mkubwa wa mwili  kutoka kilo 164 hadi kilo 124.

Takriban miezi sita iliyopita, mwanahabari huyo wa Citizen TV alifichua amepoteza kilo 30 za mwili wake, miezi miwili tangu alipoweka wazi kuwa alifanyiwa upasuaji wa kuondoa ufuta mwilini ili kupunguza uzito.

Kwenye Facebook, alionyesha jinsi mwonekano wake ulivyobadilika na na kubainisha kuwa uwekezaji mzuri alioufanya ni kwa mwili wake ili kupunguza uzito ambao ulikuwa tayari umemfanya kuonekana bonge.

“Uwekezaji wa maana zaidi ambao unaweza wekeza ni kwako wewe mwenyewe. Wakati niliamua kufanya sajari ya Bariatric, nilikuwa na woga mwingi lakini ilinibidi kufanya hivyo. Nitaelezea hadithi yangu hivi karibuni lakini mpaka sasa tayari kilo 30 zimeenda hivyo. Safari bado inaendelea,” Raburu aliandika.

Mtumbuizaji huyo mashuhuri alitumia KSh 900,000 kwa upasuaji wa gastric bypass; wakati huo, akiwa na uzito wa 164kg.

Hapo awali alikuwa amefichua kwamba ukosoaji mtandaoni na kuwa na shinikizo la damu kulichangia yeye kuamua kwenda njia ya upasuaji kufanya jitihada katika safari yake ya kupunguza uzito.

“Wakati naenda kwa upasuaji, sikuwa naendelea vizuri. Nilihitaji kwa sababu pia shinikizo langu lilikuwa juu, cholesterol yangu pia ilikuwa juu na lilikuwa suala la kuhitaji kutunza afya yangu”

Tangu afanyiwe utaratibu huo mwaka jana, mtumbuizaji huyo maarufu amekuwa akionyesha maendeleo ya safari yake ya kupunguza uzito ambayo ni wazi anajivunia.