"Ni zawadi kutoka juu" Muigizaji Celestine Gachuhi na mumewe wabarikiwa na mtoto wa kike

Muhtasari

•Celestine Gachuhi amesema kuzaliwa kwa bintiye kumeyabadilisha sana maisha yake na ya mumewe.

•Kimemia amesema bintiye ni zawadi kutoka juu na kusema sauti ya kilio chake ndiyo sauti nzuri zaidi amewahi kusikia.

Image: INSTAGRAM// PHIL KIMEMIA

Muigizaji Celestine Gachuhi na mpenzi wake Phil Kimemia wametangaza kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza.

Wawili hao wametangaza kuwa walibarikiwa na mtoto wa kike takriban wiki moja iliyopita.

Celestine ambaye anatambulika  zaidi kama Selina kutokana na kipindi 'Selina' amesema kuzaliwa kwa bintiye kumebadilisha maisha yake na ya mumewe kabisa. 

"Hata miujiza huchukua muda kidogo 😍, Binti wetu wa muujiza alikuja 😍❤️, ni wiki sasa imepita na maisha yetu yamebadilika kabisa❤️❤️🙏🙏 Phil Kimemia, namshukuru Mungu kwa ajili yako, umesimama nami tangu siku ya kwanza, katika heka heka, kama kuhani wangu. Mungu akubariki," Celestine ametangaza kupitia Instagram.

Bw Kimemia kwa upande wake amesema kuzaliwa kwa binti wao kumejenga upendo mkubwa zaidi kati yake na mkewe.

Amesema bintiye ni zawadi kutoka juu na kudai kuwa sauti ya kilio chake punde baada ya kuzaliwa ndiyo sauti nzuri zaidi amewahi kusikia.

"Hatimaye nimekutana na msichana ambaye ana sauti nzuri zaidi duniani! Siwezi kamwe kusahau hisia hiyo niliposikia ukilia, ilikuwa sauti ya kipekee zaidi, nzuri sana," Kimemia amesema.

Mwanamuziki huyo amesema kuwa mkewe alionyesha ujasiri mkubwa katika wadi ya leba alipokuwa anajifungua.

Amemhakikishia bintiye kuhusu upendo wake mkubwa kwake huku akiahidi kuwepo maishani mwake kila siku.

"Upendo sasa unahisi tofauti! Kila wakati ninapokutazama na kuona mdogo wangu na mama yako, ninazama tena kwenye upendo. Baba na mama wanakupenda sana! Wewe ni zawadi kutoka juu. Namshukuru Mungu kwa ajili yako! Ni takriban wiki moja sasa tangu ulipotua! Imma kuwa upande wako nakuahidi," Kimemia amesema.

Wapenzi hao wawili hata hivyo hawajafichua jina la binti yao.  Walitangaza habari za ujauzito wao mwezi Februari mwaka huu.