Prince Indah ashindwa kufanya shoo kutokana na ugonjwa

Wasimamizi wa Prince Indah wametangaza kuwa hatafanya shoo ambazo alikuwa amepangiwa kufanya siku kadhaa zijazo.

Muhtasari

•Malaika Musicals walisema kuwa hawawezi kufanya shoo zilizopangwa kwani Prince Indah, ambaye ndiye kiongozi wa bendi hajiskii vizuri.

•Wanamitandao wakiwemo mashabiki na wasanii wenzake Indah wameendelea kumuonyesha sapoti na kumtakia apone haraka.

Image: INSTAGRAM// PRINCE INDAH

Timu ya usimamizi ya Prince Indah, Malaika Musicals imetangaza kuwa staa huyo wa muziki wa Ohangla hatafanya shoo kadhaa ambazo alikuwa amepangiwa kufanya siku kadhaa zijazo.

Hii ni baada ya staa huyo wa Muziki wa Kiluo kushambuliwa na ugonjwa ambao haujafichuliwa hivi majuzi.

Katika taarifa yao siku ya Alhamisi, Malaika Musicals walisema kuwa hawawezi kufanya shoo zilizopangwa kwani Prince Indah, ambaye ndiye kiongozi wa bendi hajiskii vizuri.

"Tunasikitika kuwafahamisha mashabiki wetu kwamba kutokana na ugonjwa usiopangiwa wa kiongozi wa bendi yetu, PRINCE INDAH, hatuwezi kuendelea na shoo zilizopangwa katika siku kadhaa zijazo," taarifa ya usimamizi wa Prince Indah ilisoma.

Waliongeza, "Hata hivyo tutawajulisha maendeleo ya afya yake kwa wakati ufaao. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.”

Wasimamizi wa staa huyo wa Ohangla waliwaomba mashabiki kuendelea kumuombea na kuwashukuru kwa sapoti yao. Hata hivyo, hawakufichua maelezo mengi kuhusu ugonjwa uliomshambulia au alipoanza kuhisi mgonjwa.

Makumi ya wanamitandao wakiwemo mashabiki na wasanii wenzake Indah wameendelea kumuonyesha sapoti na kumtakia apone haraka.

Tazama jumbe za baadhi ya wanamitandao kwa Prince Indah;

@bahatikenya Quick recovery my brother.

@mulamwah Quick recovery.

@mauricelee001 Tupewe paybill, hatusemi pole kwa mdomo tunawire pole.

@felister_aurelian The body clearly needs a break.. quick recovery janabi.

@yycomedian Quick recovery baba

@lave.rah Pole Janabi, you are in our prayers, get well soon.