"Sasa tumerudi!" Mwimbaji Ben Githae amtema Raila Odinga na kujiunga na Kenya Kwanza

Wakati huo huo, Githae alidokeza kuhusu kujiunga na Muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Muhtasari

•Mwimbaji Ben Githae amegura rasmi kutoka muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Raila Odinga.

•DP Gachagua alimweleza mwimbaji huyo kwamba alihitaji kuomba msamaha kwa watu wa Mlima Kenya kwa kumfanyia kampeni Raila Odinga.

wakati wa mazishi ya dadake Moses Kuria, Pauline Nyokabi mnamo Januari 23.
Mwimbaji Ben Githae wakati wa mazishi ya dadake Moses Kuria, Pauline Nyokabi mnamo Januari 23.

Mwimbaji wa nyimbo za injili na za kisiasa Ben Githae amegura rasmi kutoka muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Raila Odinga.

Githae alifichua hatua hiyo siku ya Jumatatu wakati wa mazishi ya dada ya Waziri wa Biashara, Moses Kuria katika eneo la Gatundu Kusini.

Mwimbaji huyo alidokeza kwamba mwanzoni hakuwa na uhakika kuhusu ikiwa angehudhuria mazishi hayo baada ya kufahamu Rais William Ruto angekuwepo, ikizingatiwa kwamba alikuwa upande pinzani katika uchaguzi wa Agosti 2022.

"Ijumaa ndio nilienda kumtembelea mheshimiwa Moses Kuria ndipo nilijua unakuja. Nikaanza kusema nikuje tupatane ama nikose mazishi nyumbani. Lakini nikasema nitakuja nikutane nawe juu sasa imekuwa hivyo, sasa tumerudi," alisema.

Wakati huo huo, Githae alidokeza kuhusu kujiunga na Muungano tawala wa Kenya Kwanza.

"Wamuratha aliniuliza kwani hukuenda maandamano. Mimi niko hapa saizi. Huko nilihama sasa niko hapa,"

Mwimbaji huyo wa kibao 'Tena Tena' alimuomba rais Ruto kuwakaribisha waliokuwa wapinzani wake katika serikali.

"Ulienda Nyanza ukasema asilimia 99 hawakukupea ukawaambia ati njooni tusemezane na nyumbani kwako kuna majumba mengi. Sisi ni asilimia 20 ndio hatukukupea. Wacha tukuje na pia sisi tusemezane," alisema.

Huku akiongea na naibu rais, Githae alimwambia, “Riggy G si uliita wabunge wote wa Jubilee, hata wasanii ambao tulikuwa tumehama utuite. Tuko na mambo mazuri ya mlima. Hakuna wakati mwingine ambao mlima tutagawana,

Mwaka jana, Ben Githae alikuwa akimpigia debe mgombea urais wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga na alihusika sana katika kumfanyia kampeni katika eneo la Mlima Kenya ambalo lina kura nyingi.

Githae hata alimtungia wimbo kiongozi huyo wa ODM wimbo akisema  'Ndani ndani ndaniii hadi ikulu ya serikali, mlima wote baba tosha'

Wakati wa mazishi ya Jumatatu, DP Rigathi Gachagua hata hivyo alimweleza mwimbaji huyo kwamba alihitaji kuomba msamaha kwa watu wa eneo la Mlima Kenya kwa kumfanyia kampeni mgombeaji wa Azimio la Umoja.