Sonko ajawa huzuni baada ya Croatia kupigwa, sababu , Miss Croatia kuenda nyumbani

Sonko alikuwa akiipigia upato Croatia kushinda mechi hiyo na kufuzu kwa fainali

Muhtasari

•Croatia ilipigwa  na Argentina katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia ambayo ilichezwa ugani Lusail siku ya Jumanne usiku.

•Ufaransa na Morocco zitamenyana usiku wa Jumatano ili kubaini timu ambayo itaungana na Argentina kwenye fainali.

Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairoi, Mike Sonko
Image: Facebook//Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko amevunjika moyo baada ya Croatia kupigwa  na Argentina katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia ambayo ilichezwa ugani Lusail siku ya Jumanne usiku.

Timu ya Argentina ikiongozwa na nahodha Lionel Messi ilifuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia baada ya kupata ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya Croatia katika mechi ya kusisimua ambayo ilichezwa saa nne usiku.

Sonko alikuwa akiipigia upato Croatia kushinda mechi hiyo na kufuzu kwa fainali, si kwa sababu yeye ni shabiki mkubwa wa mchezo wao lakini bila shaka kwa sababu ya mashabiki wao.Shabiki mmoja aliyevutia umakini wa gavana huyo wa zamani ni Miss Croatia wa zamani, Ivana Knoll ambaye amekuwa mtu wa kuangaziwa sana katika Kombe la Dunia la mwaka huu hasa kutokana na urembo wake uliowavutia wengi.

"Katika nusu fainali hii ya kwanza ninaiunga mkono Croatia kwa sababu ya mashabiki wao lakini timu yangu ya ushindi wa kombe la Dunia la 2022 ni Morocco," Sonko alisema kwenye Facebook kabla ya mechi kuchezwa.

Matokeo baada ya dakika tisini za mechi hata hivyo hayakwenda kama jinsi Sonko alivyotaka yawe. Croatia ilipokea kichapo cha mabao matatu bila jawabu huku washambulizi wa Argentina Lionel Messi wa PSG na Julian Alvarez wa Manchester City wakifanikisha ushindi huo wao muhimu.

Messi alifunga mkwaju wa penalti katika dakika ya 34 kabla ya Alvarez kufunga bao nzuri dakika tano baadae. Argentina iliongeza chumvi kwenye kidonda cha Croatia huku Alvarez akiongeza bao la pili na la tatu kwa Argentina.

"Inasikitisha sana kwamba ny*ny*  anarudi nyumbani. Argentina sasa itacheza na Morocco katika fainali," Sonko alisema baada ya mechi kukamilika kuashiria alisikitika kufahamu kuwa huenda asimuone tena Bi Ivana.

Croatia sasa itacheza dhidi ya timu itakayopigwa katika mchuano wa leo (Jumatano)  kati ya Ufaransa na Morocco mnamo siku ya Jumamosi ili kubaini nani ataibuka nambari tatu kwenye mashindano ya mwaka huu.

Ufaransa na Morocco zitamenyana usiku wa Jumatano ili kubaini timu ambayo itaungana na Argentina kwenye fainali.