•Mama Dangote alishindwa kuficha furaha yake baada ya Tanasha Donna kumsherehekea kwa njia ya kipekee.
•Tanasha alionekana kumuomba radhi mamake Diamond kwa kuchelewa kumsherehekea mnamo siku ya kuzaliwa.
Mamake Diamond Platnumz, Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote alishindwa kuficha furaha yake baada ya mmoja wa wazazi wenza wa mwanawe, Tanasha Donna kumsherehekea kwa njia ya kipekee.
Siku ya Jumatano jioni, mamake Diamond alishiriki video za zawadi zilizoambatanishwa na ujumbe mtamu ambazo Tanasha Donna alimtumia kama njia ya kumsherehekea kwa siku yake ya kuzaliwa.
Mama Dangote alitimiza umri wa miaka 55 mnamo Julai 7 na zaidi ya miezi miwili baadaye, Tanasha hivi majuzi alimtuma zawadi ya noti za pesa zikiwa zimewekwa katikati ya maua mazuri, bidhaa za urembo na kuambatanisha kifurushi hicho na barua nzuri. Katika barua hiyo, mwimbaji huyo wa Kenya alionekana kumuomba radhi mama mkwewe wa zamani kwa kutotimiza ahadi yake ya awali.
“Mama, kitu kidogo kwa kutotimiza ahadi yangu. Natumai unaipenda. Heri ya siku ya kuzaliwa mama!! Mwenyezi Mungu akubariki daima. Upendo, T,” ujumbe kutoka kwa Tanasha ulisomeka.
Mama huyo wa mvulana mmoja pia alichora ishara kadhaa za moyo kwenye barua yake kwa Mama Dangote kuashiria upendo. Noti za pesa alizoambatanisha kwenye maua hayo zilikuwa dola za Marekani na shilingi ya Tanzania.
Katika majibu yake, Mama Dangote alionekana kuishiwa na maneno kufuatia upendo alioonyeshwa na mama huyo wa mjukuu wake na kumshukuru tu sana kwa hilo.
“Duuuh natoka zangu site nakutana na Surprise ya zawadi yangu ya birthday kutoka kwa Mama Tom kaka @tanashadonna yani sina cha kusema ila nasema Alhamdullillah,” Mamake Diamond aliandika chini ya video ya zawadi alizotumiwa na Tanasha ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Kulingana na barua aliyoandika Tanasha, mwimbaji huyo wa Kenya alionekana kumuomba radhi mamake Diamond kwa kuchelewa kumsherehekea mnamo siku ya kuzaliwa.
Tanasha Donna anaonekana kuwa na uhusiano mzuri na mamake Diamond Platnumz licha ya kutengana na staa huyo wa Bongo takriban miaka mitatu iliyopita.
Mastaa hao wa Afrika Mashariki walitengana hapo Aprili 2020 baada ya kuchumbiana kwa takriban miaka miwili. Kutengana kwao kulikuja miezi michache tu baada ya kuzaliwa kwa mtoto wao, Naseeb Abdul Jr.