Tanzia! Mcheza santuri mkongwe, DJ Lastborn ameaga dunia

Inaripotiwa kwamba Lastborn alifariki kwa amani usiku wakati akiwa amelalala.

Muhtasari

•Lastborn ambaye amekuwa akiugua kwa muda mrefu alifariki jijini Mombasa usiku wa kuamkia Ijumaa wakati akiwa amelala.

•Koikai alimtambua Lastborn kama mtu aliyekuwa makini sana katika kazi yake ya uchezaji santuri na ambaye alitaka ukamilifu.

Marehemu DJ Lastborn
Image: HISANI

Mcheza santuri mkongwe wa reggea, Benson Ouma almaarufu DJ Lastborn ameaga dunia.

Lastborn ambaye amekuwa akiugua kwa muda mrefu alifariki jijini Mombasa usiku wa kuamkia Ijumaa wakati akiwa amelala.

Habari za kifo chake zilifichuliwa na mtangazaji mashuhuri wa reggea Jahmby Koikai kwenye mtandao wa Facebook.

"Pumzika kwa amani, DJ Last Born. Rafiki yangu, mwalimu wangu, na mshirika wangu wa muziki. Nilikuwa na bahati ya kukutana nawe muda mfupi baada ya shule ya upili katika klabu ya Hollywood na muunganisho wetu kupitia muziki ulikuwa wa papo hapo. Ulinifundisha jinsi ya kuwa DJ na kwa pamoja tukaunda Supremacy Sounds," Njambi aliandika.

"Athari yako kwa maisha yangu na shauku yetu iliyoshirikiwa haitasahaulika kamwe. Utakumbukwa kila wakati kama mtu mwenye talanta ya kweli na rafiki mpendwa. Pumzika kwa amani rafiki yangu,

Mtangazaji huyo alimtambua Lastborn kama mtu aliyekuwa makini sana katika kazi yake ya uchezaji santuri na ambaye alitaka ukamilifu.

"Wengi wetu kutoka enzi hiyo, tumekuwa na mgao wetu wa kutosha wa masomo ya maisha na uzoefu kutoka kwa maswala mazito ya kiafya hadi mageuzi ya tasnia. Naomba neema, nguvu na uongozi wa Mungu," alisema.

Inaripotiwa kwamba Lastborn alifariki kwa amani usiku wakati akiwa amelalala.

Mcheza santuri huyo amekuwa akiugua kwa muda mrefu baada ya kukumbwa na maradhi ya kiharusi mara mbili. Kiharusi cha mwisho kilichomkumba takriban miaka mitatu iliyopita jicho na uwezo wake wa kuongea.

Amekuwa akishughulikiwa na dada yake jijini Mombasa hadi kufariki kwake siku ya Ijumaa.