Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kwa sasa yuko jijini Boston, Marekani ambapo amepata fursa ya kukutana na watoto wake baada ya muda mrefu.
Haijabainika wazi ni lini mwanamuziki huyo mahiri wa Kikuyu alitua katika nchi hiyo ya Magharibi lakini bintiye Shirleen Muchoki alifichua habari kuhusu mkutano wao.
Malkia huyo mdogo alitumia ukurasa wake wa Instagram kuelezea furaha yao kwa kukutana na mzazi huyo wao na kufunguka jinsi walivyompeza.
"Wow, siku nzuri sana, baba yangu hatimaye yuko hapa, tumeku’miss baba, karibu Boston," Shirleen alisema katika chapisho lake la Jumatatu asubuhi.
Alionyesha picha nzuri za mwimbaji huyo Mugithi akishiriki wakati mzuri pamoja naye na kaka yake mdogo kwenye uwanja wa ndege. Bi Edday Nderitu na mtoto wao mdogo zaidi hata hivyo hawakuonekana popote kwenye picha, haijabainika iwapo walikuwa pale.
Huenda hii ndiyo mara ya kwanza kwa Samidoh kukutana na watoto wake baada ya miezi mingi sana.
Mke wa kwanza wa mwanamuziki huyo, Bi Edday Nderitu aligura Kenya na kuhamia Marekani pamoja na watoto wao watatu mapema mwaka jana kufuatia drama nyingi zilizoingia katika ndoa yao ya zaidi ya mwongo mmoja.
Mwezi Julai, mama huyo wa watoto watatu aliweka wazi kwamba alimuacha mume wake ili awe na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.
"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.
Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."
Alibainisha kuwa hajutii uamuzi wa kugura ndoa yake na akaweka wazi ameweza kuendelea kuwalea watoto wake bila usaidizi wowote.