Muigizaji Fridah Kajala Masanja anaendelea kupata nafuu baada ya kushambuliwa na ugonjwa ambao haujafichuliwa siku kadhaa zilizopita.
Katika kipindi cha siku chache zilizopita kumekuwa na madai yasiyothibitishwa kwamba mama huyo wa binti mmoja hajisikii vizuri lakini wanamitandao wamekuwa wakikisia tu kuhusu nini kinaweza kuwa tatizo.
Alhamisi asubuhi hata hivyo mchumba wake Harmonize alithibitisha kuwa anaugua na kumtakia apone haraka.
"Pona haraka mpenzi. Siwezi kusubiri kukuona ukiwa mwenye nguvu tena," staa huyo wa Bongo aliandika chini ya picha ya Kajala akionekana mdhaifu ambayo alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Pichani, muigizaji huyo anaonekana akiwa amekaa chini na kuinama kidogo huku akiwa ameweka mikono yake pamoja.
Mapema wiki hii Kajala alidokeza kuwa ni mgonjwa baada ya kuchapisha video fupi ambayo ilionyesha sindano iliyodungwa kwenye mkono wake. Hata hivyo, hakufichua maelezo zaidi na kuwaacha watu kukisia anaugua nini.
Wakati mjadala kuhusu ugonjwa wa Kajala ukitikisa ulimwengu wa Bongo, uvumi kuhusu ujauzito pia uliibuka. Aliyekuwa chawa wa Harmonize, Mwijaku aliibua madai mazito kuhusu muigizaji huyo kuwa hakutaka 'ujauzito' huo.
"Tayari dada yetu ameenda kutoa ujauzito, ameona wanapo elekea ni uneconomic freedom kwa familia na yeye yupo after pesa," alisema.
Matamshi ya Mwijaku yalizua mjadala mkubwa Bongo ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu amekuwa na ukaribu mkubwa na bosi huyo wa Konde Music Wordwide kabla ya kutengana kwao mwezi uliopita.
Wiki kadhaa zilizopita mtangazaji huyo alionekana kumgeuka Harmonize na kuibua mzozo wa wazi naye. Siku za hivi majuzi amekuwa akijihusisha sana na Diamond ambaye pia ni boss wake katika Wasafi Bet.
Harmonize na Kajala wamekuwa pamoja kwa takriban nusu mwaka baada ya kurudiana mapema mwaka huu. Wapenzi hao walirudiana mwezi Mei baada ya juhudi nyingi za Harmonize za kuomba msamaha.